Oct 11, 2017 04:53 UTC
  • Rouhani: Kuanzishwa vita hakutainufaisha nchi yoyote Mashariki ya Kati

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuhusu taathira hasi za kuanzishwa vita na kuibuliwa mifarakano zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumanne katika mazungumzo yake na Karen Karapetyan, Waziri Mkuu wa Armenia hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kuna udharura kwa nchi zote za eneo hili kufanya hima kuhakikisha kuwa amani ya kudumu na uthabiti unapatikana.

Akiashiria kuhusu migogoro iliyopo sasa hivi katika baadhi ya nchi za eneo kama vile Syria, Yemen na Iraq, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kupatiwa ufumbuzi mizozo hiyo kutakuwa ni kwa maslahi ya nchi zote za eneo.

Wakati huo huo, Rais Hassan Rouhani amesema Iran na Armenia zina misimamo inayofanana katika masuala ya kieneo na kimataifa, na jambo hilo linaweza kutumiwa kutafutiwa ufumbuzi migogoro iliyopo, huku akisisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili.

Bendera za Iran na Armenia

Kwa upande wake, Karen Karapetyan, Waziri Mkuu wa Armenia amesema misimamo ya wastani ya Iran katika masuala ya eneo imetoa dhamana na matumaini ya kupatikana amani na uthabiti Mashariki ya Kati.

Kadhalika amezitaka Tehran na Yerevan kutumia fursa zilizopo kuimarisha uhusiano wa pande mbili, na hususan ushirikiano katika sekta za biashara na uchumi.

Waziri Mkuu wa Armenia ambaye aliwasili hapa nchini Jumatatu kwa ziara rasmi ya kikazi, amesaini hati tatu ya maelewano na maafisa wa ngazi za juu wa Iran, ambayo imegusia juu ya kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili katika sekta za tiba ya mifugo, mabadilishano katika nyuga za sanaa, utamaduni, sayansi na teknolojia.

Tags