Jan 14, 2018 07:56 UTC
  • Larijani: Iran daima ina hamu ya kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Jamhuri ya Kiislamu ina hamu kubwa ya kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika.

Ali Larijani aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkutano na Privat Oula, Naibu Spika wa Bunge la Ivory Coast hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Mkutano wa 13 wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu (OIC) ni jukwaa zuri la kuandaa mazingira ya kuimarisha uhusiano huo.

Dakta Larijani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Kodivaa katika nyuga mbalimbali.

Mkutano wa Mabunge ya nchi wanachama wa (PUIC) Tehran

Kadhalika ameashiria changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na kubainisha kuwa, mikutano kama huu wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu PUIC unaondelea hapa Tehran, inafaa kutumiwa kujadili na kuitafutia ufumbuzi migogoro inayoshuhudiwa katika nchi kama vile Myanmar na Palestina, sanjari na masuala nyeti kama ugaidi.

Kwa upande wake Privat Oula, Naibu Spika wa Bunge la Ivory Coast amesema nchi yake ipo tayari kuunga mkono misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuwa nchi mbili hizi zimekuwa na mtazamo mmoja katika masuala ya ulimwengu wa Kiislamu kwa muda mrefu.

Amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi yake na Iran katika nyuga za uchumi na mabunge, huku akimualika Dakta Larijani kuitembelea nchi yake.

 

Tags