Iran yavunja rekodi katika uuzaji wa gesi ya LPG Afrika, Asia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweka rekodi mpya katika uuzaji wa gesi aina ya LPG katika nchi kadhaa za mabara ya Afrika na Asia ambapo iliuza tani 520,000 Januari mwaka huu hilo likiwa ni ongezeko la asilimai 39.4 kutoka mwezi uliotangulia.
Nchi za bara Asia zinazonunua gesi la LPG kwa wingi kutoka Iran ni pamoja na China, India, Taiwan na Indonesia, Thailand na Pakistan.
Halikadhalika nchi za Afrika zinazonunua gesi ya LPG ya Iran kwa wingi Afrika ni pamoja na Kenya, Afrika Kusini na Tanzania.
Hayo yanajiri huku kukiripotiwa ongezeko la mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Kenya.
Kwa mujibu wa Murtadha Daylan, mwambata wa kibiashara wa Iran mjini Nairobi, "Kenya ni nchi ya 15 inayonunua kwa wingi bidhaa kutoka Iran kwa mujibu wa takwimu za mwezi Machi mwaka 2017."
Afisa huyo wa masuala ya kibiashara katika ubalozi wa Iran nchini Kenya amesema kati ya mipango ya baadaye ni kuundwa chumba cha kibiashara cha pamoja baina ya Iran na Kenya kwa ajili ya kubadilishana habari na kupunguza matatizo ya kibiashara baina ya pande mbili.