Zarif: Msingi wa kifikra, kifedha wa ISIS bado haujaangamizwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40811-zarif_msingi_wa_kifikra_kifedha_wa_isis_bado_haujaangamizwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, msingi wa kifikra na kifedha wa kundi la magaidi wakufurishaji wa Daesh au ISIS ungalipo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 24, 2018 10:40 UTC
  • Zarif: Msingi wa kifikra, kifedha wa ISIS bado haujaangamizwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, msingi wa kifikra na kifedha wa kundi la magaidi wakufurishaji wa Daesh au ISIS ungalipo.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo mjini Tehran katika 'Kongamano la Kimataifa la Muelekeo wa Kieneo Baada ya ISIS' na kuongeza kuwa, ISIS bado ipo Asia Magharibi na maeneo mengine.

Zarif ameendelea kusema kuwa: 'Uingiliaji wa madola ya kigeni ndio moja ya sababu kubwa zaidi za kukosekana usalama na kuendelea kubakia fikra za ISIS katika eneo la Asia Magharibi. Ameongeza kuwa,  hata baada ya kufurushwa magaidi wakufurishaji wa ISIS kutoka ardhi walizokuwa wakizikalia lakini msingi wa kifikra na kifedha upo na pia mazingira yaliyopelekea kuibuka kundi hilo bado yapo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, ISIS iliibuka kutokana na hujuma ya kijeshi ya  Marekani dhidi ya Iraq. Aidha amesema sababu nyingine ya kuibuka ISIS ni kushindwa ulimwengu wa Kiarabu kuunda serikali ya kitaifa na kutozingatia matakwa ya wananchi. Hali kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema baadhi ya serikali za kieneo kama vile Saudi Arabia zimenajaribu kuhamishia nje ya nchi matatizo yao ya ndani ya nchi. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif akihutubia kikao kuhusu  'Kongamano la Kimataifa la Muelekeo wa Kieneo Baada ya ISIS', Tehran, 24/02/2018

Zarif amesema fikra za ISIS ni tishio kubwa kwa eneo na dunia kwa ujumla na kuongeza kuwa, wafuasi wa ISIS ambao hawakuangamizwa sasa wanasambaa katika eneo hasa nchini Afghanistan na maeneo mengine duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria mpango wa Iran kuhusu kuundwa jumuiya ya mazungomzo ya kieneo katika Ghuba ya Uajemi na kusema: "Baadhi ya nchi za eneo zinataka kuleta usalama katika eneo kwa msingi wa kuunda muungano dhidi ya Iran." Amesema nchi hizo zinatumia kiasi kikubwa cha fedha kujihami kwa silaha kwa dhana kuwa zitapata usalama katika hali ambayo usalama unapaswa kuwepo kwa msingi wa mazungumzo.