Zarif: Iran itafuata nyayo iwapo US itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43620
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuna uwezekano mkubwa Iran itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, iwapo Marekani itaamua kujivua kwenye mapatano hayo ya kimataifa ya mwaka 2015.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 25, 2018 07:34 UTC
  • Zarif: Iran itafuata nyayo iwapo US itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuna uwezekano mkubwa Iran itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, iwapo Marekani itaamua kujivua kwenye mapatano hayo ya kimataifa ya mwaka 2015.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press mjini New York jana Jumanne, Mohammad Javad Zarif amesema iwapo Rais Donald Trump atatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran, atakuwa 'ameua mapatano hayo' na Tehran haitalazimika kufungamana na masharti na mipaka ya makubaliano hayo yaliyofikiwa mjini Vienna Julai mwaka 2015.

Dakta Zarif amekosoa vikali vitisho vya kujikariri dhidi ya Iran vilivyotolewa jana na Trump katika kikao na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron kwamba mapatano hayo ni mabaya na yemejengeka kwenye misingi iliyooza, na kwamba lazima masuala kadhaa yaangaliwe upya.

Marais wa Marekani na Ufaransa

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amebainisha kuwa, hatua yoyote ya kiuhasama na ya kukiuka makubaliano hayo itamaanisha kuwa, mazungumzo yajayo kati ya Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini hayatakuwa na maana kwani Washington itakuwa imedhihirisha kuwa sio mshirika wa kuaminika. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ina machaguo kadhaa ya kuchukua iwapo Marekani itajiondoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia, ikiwemo kujiondoa kwenye mkataba wa NPT unaozuia utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa silaha za atomiki, sambamba na kuanzisha upya shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani lakini kwa kasi ya juu.