Shauku ya Pakistan ya kustawisha zaidi uhusiano wa kibiashara na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i47260-shauku_ya_pakistan_ya_kustawisha_zaidi_uhusiano_wa_kibiashara_na_iran
Mkuu wa Chama cha Tehreek-e-Insaf cha Pakistan ambacho hivi karibuni kiliibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge, kwa mara nyingine tena ametangaza utayari wake wa kustawisha uhusiano wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 06, 2018 02:40 UTC
  • Shauku ya Pakistan ya kustawisha zaidi uhusiano wa kibiashara na Iran

Mkuu wa Chama cha Tehreek-e-Insaf cha Pakistan ambacho hivi karibuni kiliibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge, kwa mara nyingine tena ametangaza utayari wake wa kustawisha uhusiano wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Imran Khan, Waziri Mkuu mtarajiwa wa Pakistan amesema hayo katika mazungumzo yake na Mehdi Honardoost balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Islamabad na kutaka kustawisha zaidi uhusiano na nchi zote jirani ikiwemo Iran kwa lengo la kujitosheleza kiuchumi. Licha ya kuwa chama cha Imran Khan ambaye ni nyota wa zamani wa mchezo wa Kriketi cha Tehreek-e-Insaf kimeibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge wa hivi karibuni nchini Pakistan, lakini hakijaweza kupata ushindi mutlaki ambao kikatiba unakipa uwezo wa kuunda serikali.

Hivyo chama hicho kinalazimika kuungana na chama kingine kwa ajili ya kuunda serikali. Ndio maana chama cha Imran Khan kimefikia makubaliano na chama cha Muttahida Qaumi Movement-Pakistan (MQM) na muda si mrefu serikali mpya ya Pakistan itaundwa na kuanza kazi zake. Aidha Imran Khan anatarajiwa kuapishwa hivi karibuni kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ambapo tayari ametangaza kuwa, serikali yake inalipa kipaumbele suala la kustawisha uhusiano na majirani hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jambo hilo lina umuhimu kwa serikali ya Islamabad kwa mambo kadhaa. 

Imran Khan, Mkuu wa chama cha Tehreek-e-Insaf 

Mosi ni kuwa, Pakistan ina mpaka wa pamoja na nchi tatu za Iran, India na Afghanistan. Ukiacha uhusiano wake mzuri na Iran, nchi ya Pakistan ina uhusiano unaolegalega na nchi mbili zilizobakia yaani India na Afghanistan.  Ni kwa sababu hiyo ndio maana Pakistan inaiona Iran kama ni stratejia yake kubwa na muhimu.

Nukta ya pili ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina akiba kubwa ya gesi na mafuta na siku zote imekuwa ikitangaza utayari wake wa kuidhaminia Pakistan nishati katika nyuga zote ikiwemo sekta ya umeme. Umuhimu wa tatu wa Iran kwa Pakistan ni nafasi muhimu ya Tehran katika kudhamini usalama na uthabiti wa eneo la Mashariki ya Kati, kiasi kwamba, Iran inatajwa kuwa nanga ya uthabiti wa eneo.

Nafis Zakaria mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Pakistan anasema kuwa: "Kupambana na ugaidi ni moja ya nyanja za ushirikiano baina ya nchi mbili rafiki na jirani za Pakistan na Iran na ushirikiano huu wa pande mbili ni ishara njema ya mustakabali mwema kwa ajili ya eneo hili."

Chama cha Tehreek-e-Insaf 

Kwa mtazamo wa duru za kisiasa nchini Pakistan ni kuwa, kile ambacho ni muhimu ni kutekelezwa mchakato wa kustawisha uhusiano wa nchi hiyo na Iran hususan katika sekta ya nishati ya gesi. Licha ya kuwa Pakistan inahitajia mno gesi na Jamhuri ya Kiislamu imeanzisha katika mpaka wa Pakistan njia ya kupeleka gesi katika nchi hiyo, lakini kutokana na serikali iliyopita kutoa kipaumbele zaidi cha kuwa na uhusiano na Marekani, hakukuchukuliwa hatua za maana kwa ajili ya kufanikisha hilo.

Kwa muktadha huo, hatua ya Imran Khan ya kutangaza kuwa na shauku na hamu ya kupanua uhusiano na Tehran imeleta matumaini katika jamii ya Pakistan kwamba, Waziri Mkuu huyo mtarajiwa atatekeleza kivitendo mkataba Iran wa kuiuzia gesi Pakistan.

Mhariri wa gazeti la Nawa-i-Waqt la Pakistan ameandika katika toleo la hivi karibuni kwamba:

"Ili kutekeleza kivitendo mpango wa kusafirisha gesi, Iran ilikwenda mbali zaidi na kupendekeza kuweko mradi wa pamoja ndani ya ardhi ya Pakistan, lakini viongozi wa Islamabad ambao wanadai kuwa na mamlaka na kutosikiliza maneno na amri za Marekani walinyamaza kimya. Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu nchini Pakistan inaongezeka sambamba na kuongezeka mahitaji ya nishati hiyo katika nchi hiyo."

Ujenzi wa mabomba ya kusafiriishia gesi ya Iran kuelekea Pakistan

Alaa Kulli haal, kukaribisha kwa mikono miwili duru za kieneo na kimataifa ushindi wa chama cha Imran Khan cha Tehreek-e-Insaf katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Bunge nchini Pakistan ni ishara njema za kufunguliwa ukurasa mpya wa kupanua ushirikiano baina ya pande mbili na pande kadhaa katika nyanja zote.

Imran Khan  pia ambaye ushindi wake unahesabiwa kuwa ni mabadiliko makubwa na ya kihistoria tangu Pakistan ipate uhuru mwaka 1947, anapaswa kutumia vyema fursa hii na asibadilishe matumaini ya wananchi ya kupatiwa ufumbuzi matatizo ya kiuchumi na kuwa hali ya kukata tamaa.

Bila shaka kurekebisha uhusiano na kuweko hali ya uwiano katika uhusiano wa Islamabad na nchi zenye taathira muhimu kwa matukio ya eneo, ni jambo ambalo litakuwa na taathira muhimu katika kudhamini maslahi ya kitaifa ya Pakistan.