Sep 22, 2018 08:15 UTC
  • Hujuma ya kigaidi katika mji wa Ahvaz kusini mwa Iran

Magaidi wametekeleza hujuma ya kigaidi wakati wa kufanyika gwaride ya majeshi ya Iran katika mji wa Ahvaz kusini mwa Iran.

Mkuu wa Mkoa wa Khuzestan Gholamreza Shariati amesema wakati wa Gwaride ya Majeshi ya Iran magaidi waliokuwa wamevalia sare bandia za kijeshi walianza kufyatua risasi upande wa jukwaa na pia sehemu walikokuwa wananchi. Katika hujuma hiyo watu kadhaa wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto wameuawa shahidi au kujeruhiwa.

Shariati amesema hadi sasa watu watatu wamethibitishwa kuuawa shahidi na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa. Amesema usalama kamili sasa umerejea katika eneo hilo. Aidha Shariati amesema kundi la kigaidi ambalo limetekeleza hujuma hiyo limeangamizwa na kwamba maafisa wa usalama wako katika hali ya tahadahri.

Maafisa wa usalama wakiwasaidia watoto waliokuwa katika eneo la gwaride

Kundi la magaidi wakufurishaji waliotekeleza shambulizi hilo la leo mjini Ahvaz linapata himaya ya Uingereza na Saudia Arabia. Hujuma hiyo ni sehemu ya miradi ya kuibua ghasia na machafuko na kueneza hali ya kutokuwa na matumani nchini Iran. Miradi hiyo ilianza kutekelezwa katika msimu wa joto lakini imefeli na ndio sababu watekelezaji wake wameamua kutekeleza hujuma za kigaidi.

Tags