Iran: Israel itajuta kwa kuwaunga mkono magaidi na kuishambulia Syria
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuendelea kuzishambulia ngome za jeshi la Syria na waitifaki wake na kusisitiza kuwa, Tel Aviv itakabiliwa na jibu kali iwapo haitasitisha uvamizi wake na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Ali Shamkhani ametoa onyo hilo leo Alkhamisi hapa mjini Tehran, katika mazungumzo na mwenzake wa Russia, Nikolai Patrushev na kubainisha kuwa, iwapo Israel haitaacha chokochoko zake hizo, basi ijiandae kupokea jibu kali litakaloifanya ijute.
Kadhalika ameashiria kuhusu hatua ya Marekani ya kuziwekea vikwazo Iran, China na Russia na kusisitiza kuwa, kitendo hicho cha Washington kimechochewa na matatizo yanayoukumba utawala wa Rais Donald Trump na kwamba Tehran, Moscow na Beijing zitaendelea kushirikiana ili kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani.
Kwa upande wake, ofisa huyo wa ngazi ya juu wa usalama wa Russia amesema kutoichukulia hatua Marekani kutaifanya iendeleze sera zake hizo za upande mmoja na za ubeberu ambazo zimeitumbukiza dunia katika migogoro kama ile inayoshuhudiwa Syria, Iraq na Afghanistan.
Mgogoro wa Syria ulizushwa mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yenye aidolojia ya Uwahabi na yanayoungwa mkono na Marekani, Israel, Saudia, na baadhi ya nchi kuanzisha mashambulizi makali kwa lengo la kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.
Hata hivyo njama hizo chafu zimefeli kutokana na kusimama imara wananchi wa Syria pamoja na ushirikiano wa Iran, Raussia, Syria na harakati ya muqawama ya Hizbullah ya nchini Lebanon katika kukabiliana na magenge hayo ya kigaidi.