Nov 04, 2018 08:10 UTC
  • Larijani: Trump ni mdogo sana, hawezi kuipigisha magoti Iran

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Rais Donald Trump wa Marekani ni 'mdogo sana' kuweza kufanikiwa kulipigisha magoti taifa la Iran.

Ali Larijani ameyasema hayo hii leo katika kikao cha Bunge kwa mnasaba wa kumbukumbu ya tarehe 13 Aban inayosadifiana na tarehe 4 Novemba, ambayo inajulikana hapa nchini kama “Siku ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa" na "Siku ya Mwanafunzi" inayoadhimishwa hii leo. 

Amesema "Marekani iwe na uhakika kwamba Wairani watamuonesha Trump namna alivyo mdogo na asivyoweza kufanikiwa kulipigisha magoti taifa hili."

Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran

Ameongeza kuwa, namna Wairani walivyomtimua mbio dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein, na namna walivyokata pumzi za mamlumki wa kigaidi wa Daesh (ISIS) wanaoungwa mkono na Marekani, vivyo hivyo watawajutisha wakazi watenda jinai wa Ikulu ya White House.

Katika hatua nyingine, wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka kila pembe ya Iran hii leo wamejitokeza kwa wingi katika maandamano ya kuadhimisha "Siku ya Kutekwa Pango la Ujasusi". Hapa Tehran maandamano hayo yamefanyika nje ya jengo lililokuwa na ubalozi wa Marekani, na yameshuhudiwa pia katika miji mingine zaidi ya elfu moja nchini.

Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba vibonzo vya kumkejeli Trump na bendera za Marekani, huku wengine wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe zinazosema: "Mauti kwa Marekani...Mauti kwa Wazayuni...Marekani inafanya Ugaidi wa Kiserikali....na Katu Hatukubali Udhalilishwaji."

Wanawake katika maandamano dhidi ya Marekani mjini Tehran

Itakumbukwa kuwa, tarehe 4 Novemba mwaka 1979, wanafunzi wa Iran katika kulalamikia njama za Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran walivamia na kuzingira 'Pango la Ujasusi'  yaani (Ubalozi wa Marekani) mjini Tehran kwa lengo la kuzuia dola hilo la kibeberu kufikia malengo yake haramu dhidi ya mapinduzi machanga yaliyokuwa yamefikia ushindi Februari mwaka huo. 

 

Tags