"Orodha ya vikwazo vipya dhidi ya Iran vinaonesha kukanganyikiwa Marekani"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49322-orodha_ya_vikwazo_vipya_dhidi_ya_iran_vinaonesha_kukanganyikiwa_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema miongoni mwa majina yaliyoko kwenye orodha ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Tehran ni benki iliyofungwa miaka sita iliyopita na meli ya mafuta ya Iran iliyozama katika bahari ya China karibu mwaka mmoja uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 06, 2018 04:36 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema miongoni mwa majina yaliyoko kwenye orodha ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Tehran ni benki iliyofungwa miaka sita iliyopita na meli ya mafuta ya Iran iliyozama katika bahari ya China karibu mwaka mmoja uliopita.

Mohammad Javaz Zarif amesema hatua hiyo ya Washington ya kuziwekea vikwazo taasisi ambazo hazipo tena kunaonesha wazi namna utawala huo wa kibeberu ulivyokanganyikiwa na kuwa na pupa ya kuchukua hatua hasi dhidi ya Iran.

Dakta Zarif ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Benki ya Tat iliyoanishwa kwenye orodha ya vikwazo vipya vya Marekani ilifilisika miaka sita iliyopita na kisha kufungwa, na meli ya mafuta iliyoorodheshwa ni ile iliyozama katika ajali iliyotokea katika bahari ya China.

Januari mwaka huu, meli ya mafuta ya Iran, MV Sanchi ilizama katika Bahari ya China Mashariki baada ya kugongana na meli nyingine na kuwaka moto kwa muda wa wiki moja, ambapo wahudumu wote 32 wa meli hiyo walipoteza maisha yao.

Benki za Tat za Iran zilifungwa mwaka 2012 baada ya kufilisika

Hapo jana Marekani ilianza kutekeleza awamu nyingine ya vikawzo vyake vya kidhalimu dhidi ya Iran ambavyo vinajumuisha sekta ya benki, mabadilishano ya kifedha na uuzaji wa mafuta ya Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kwamba, vikwazo hivyo vipya ni muendelezo wa vita vya kisaikolojia vya Washington dhidi ya wananchi wa Iran na katu havitafua dafu kwa maslahi ya Marekani.