Ujumbe wa Zarif; vikwazo na kufedheheka Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49347-ujumbe_wa_zarif_vikwazo_na_kufedheheka_marekani
Akizungumza jana ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kutekelezwa duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amewahutubu viongozi wa Washington kwa kusema, serikali ya Marekani ambayo imeshindwa hata kuwathibitishia wananchi wake kwamba, sera zake ni kwa munufaa ya wananchi inasubiriwa na hatima mbaya katika siku za usoni.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 07, 2018 04:46 UTC
  • Ujumbe wa Zarif; vikwazo na kufedheheka Marekani

Akizungumza jana ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kutekelezwa duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amewahutubu viongozi wa Washington kwa kusema, serikali ya Marekani ambayo imeshindwa hata kuwathibitishia wananchi wake kwamba, sera zake ni kwa munufaa ya wananchi inasubiriwa na hatima mbaya katika siku za usoni.

Dakta Muhammad Javad amesema katika ujumbe wake kwa taifa la Iran kwa njia ya vidio kwamba: Wananchi watengenezaji historia wa Iran ambao wameonyesha kwamba, wameweza kubadilisha njia ya matukio ya kihistoria kwa juhudi na kujiamini na kwa kusimama kidete, mara hii pia watakariri tajiriba na uzoefu huo, na Wamarekani watajutia hatua za pupa na zisizo za busara zilizochukuliwa na serikali ya Donald Trump. 

Awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani ambayo inajumuisha sekta ya mafuta, benki na mabalishano ya kibiashara na Iran ambayo kimsingi inawalenga moja kwa moja wananchi, ilianza kutekelezwa juzi Novemba 5. Vikwazo hivyo vimepuuza kabisa ada za kimaadili na za kimataifa. Hatua za kukiuka sheria na za upande mmoja za Rais Donald Trump wa Marekani zinaweka wazi ukweli huu kwamba, Trump anafanya harakati kinyume kabisa na matakwa ya walimwengu.

Rais Donald Trump wa Marekani

Msingi wa harakati hizo za Trump umejengeka juu ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ambapo kuendelea mwenendo huu ni tishio kwa ulimwengu. Matokeo ya serikali ya Trump ya kupuuza na kukiuka sheria za kimataifa na kutanguliza mbele ubabe na utumiaji mabavu, hayaiathiri Iran tu bali yanaziathiri nchi nyingine pia za ulimwengu. Mfano wa wazi wa hilo ni hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris Ufaransa na vita vyake vya kibiashara.

Katika uwanja huo, Mohammad Kazem Sajjadpour, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kisiasa na Masuala ya Kimataifa cha Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran  anasema kuwa: Serikali ya Marekani inajiona iko juu ya viongozi wa Ulaya. Bila shaka viongozi wa Ulaya wanapaswa kuchukua hatua za haraka kwa minajili ya kukabiliana na miamala ya upande mmoja ya Marekani.

Kuwa pamoja walimwengu dhidi ya siasa haribifu za Donald Trump ambazo zilianza baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kunahitajia hatua za kivitendo zaidi ili kuizuia serikali ya sasa ya Marekani kuendelea kuzungumza na walimwengu kwa lugha ya vita baridi. 

Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza juu ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili

Hivi sasa  barani Ulaya, Asia na Afrika kumejitokeza kila ishara za kupinga siasa za kibabe za Marekani. Akibainisha kwamba, Uturuki haitafuata na kutekeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo alisema jana kuwa: Vikwazo hivi ni kinyume na sheria za kimataifa na diplomasia ya kimataifa. Watu wote wanataka kuishi katika dunia yenye amani; na hawataki kuishi katika dunia ya ubabe na ubeberu.

Utendaji huu ndio umekuwa mkondo wa serikali na taifa la Iran tokea baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na tajiriba ya miongo minne ya mapinduzi haya imethibitisha kwamba, taifa la Iran katu si lenye kusalimu amri mbele ya ubabe na utumiaji mabavu. Kwa kuzingatia tajiriba na uzoefu huu wa kihistoria, Dakta Muhammad Javad Zarif alisisitiza katika ujumbe wake kwa taifa la Iran kwamba, taifa hili likitegemea kusimama kwake kidete na mamlaka yake ya kujitawala kwa mara nyingine tena litaifanya serikali ya Trump ijute kama ilivyokuwa kwa serikali zilizotangulia za Marekani.

Imani, kujiamini na kuwa na moyo wa kupigania kujitawala na kupinga dhulma na uonevu, ni sifa muhimu za taifa la Iran zinazojulikana baina ya walimwengu. Sifa hizi zilidhihirika zaidi na kuwa na thamani kubwa zaidi katika historia na katika kipindi nyeti cha uhai wa Mapinduzi ya Kiislamu kikiwemo kile kipindi cha vita vya kichokozi vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein.

Rais Rouhan: Iran itavishinda vikwazo vya Marekani kwa msaada na ushirikiano wa wananchi

Kanali ya Televisheni ya Sky News ilitangaza jana ikiwanukuu weledi wa mambo kwamba: Kile ambacho kinatajwa kama vikwazo vikali kabisa vya Marekani, hakitaipigisha magoti Iran na katu vikwazo hivyo haviwezi kuifanya Tehran iende mbele ya Washington ikiwa imeinamisha kichwa.

Orodha ndefu ya vikwazo vya Marekani iliyotangazwa tarehe 5 Novemba ambamo ndani yake ilikuwa na makosa na kuonyesha kuchanganyikiwa Washington inaonyesha kuwa, kusimama kidete taifa la Iran kwa ajili ya kutetea thamani za mapinduzi yake ya Kiislamu, kumewakasirisha mno viongozi wa Marekani; taifa ambalo halitaki kudunishwa ambapo licha ya magumu yote lakini limeendelea kusimama kidete na kutotetereka hata kidogo mbele ya wababe na mabeberu.