Zarif: Vikwazo vya Marekani havitaiburuza mezani Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49634-zarif_vikwazo_vya_marekani_havitaiburuza_mezani_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya kidhalmu vya Marekani katu haviwezi kuilazimisha Tehran iende kwenye meza ya mazungumzo wala kuifanya isalimu amri mbele ya matakwa ya Washington.
(last modified 2026-02-24T04:35:04+00:00 )
Nov 20, 2018 08:06 UTC
  • Zarif: Vikwazo vya Marekani havitaiburuza mezani Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya kidhalmu vya Marekani katu haviwezi kuilazimisha Tehran iende kwenye meza ya mazungumzo wala kuifanya isalimu amri mbele ya matakwa ya Washington.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la The Guardian la Uingereza na kufafanua kuwa, duru mpya ya vikwazo hivyo dhidi ya Iran sio tu haitakuwa na taathira yoyote kwa taifa la Iran, bali italifanya listawi zaidi. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu amekumbusha kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi sasa umeshatoa ripoti chungunzima zenye kuthibitisha kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani na kuongeza kwamba, bila shaka mafuta ya Iran yanaendelea kupata soko licha ya vikwazo hivyo.

Hapo jana pia Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, taifa hili litabakia kuwa huru na lenye mamlaka yake na katu halitasalimu amri mbele ya Marekani.

Awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo ilianza kutekelezwa tarehe 7 Agosti na awamu ya pili ilianza kutekelezwa rasmi tarehe 5 Novemba.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kujitoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran.

Jamii ya kimataifa imekosoa vikali maamuzi hayo ya Trump ambapo Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya zimetangaza kufungamana na JCPOA.