Iran: Safari ya kinyemela ya Trump Iraq ni kuwakosea heshima Wairaq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50483-iran_safari_ya_kinyemela_ya_trump_iraq_ni_kuwakosea_heshima_wairaq
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema safari ya siri na ya kushtukiza ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Iraq imekiuka misingi yote ya udiplomasia na ni kutoheshimu uhuru wa kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 29, 2018 01:07 UTC
  • Iran: Safari ya kinyemela ya Trump Iraq ni kuwakosea heshima Wairaq

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema safari ya siri na ya kushtukiza ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Iraq imekiuka misingi yote ya udiplomasia na ni kutoheshimu uhuru wa kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.

Bahram Qassemi aliyasema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa: Licha ya uingiliaji wa Marekani usiokuwa na hesabu na kupoteza maelfu ya mabilioni ya dola kwa ajili ya uwepo wake katika eneo hili kinyume cha sheria haswa Iraq, lakini Trump analazimika kuitembelea moja ya nchi za eneo kinyemela, kwa kificho na chini ya ulinzi mkali.

Amesema safari hiyo ya Trump haijalalamikiwa tu wananchi wa Iraq, lakini pia imekosolewa vikali na weledi wa mambo katika pembe zote za dunia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, "Ni kuwa macho mataifa ya eneo - na si tamaa na uungaji mkono wa Marekani kwa magaidi - ndiko kulikowezesha kukatwa mizizi ya magenge ya kigaidi yaliyoundwa na kuungwa mkono kwa hali na mali na Marekani na utawala wa Kizayuni."

Trump pamoja na askari wa Marekani nchini Iraq

Bahram Qassemi sanjari na kulaani uropokaji wa Trump alipokuwa Iraq, amebainisha kuwa, serikali na mataifa ya eneo hili katu hayatakubali maajinabi wapalilie mbegu za mifarakano miongoni mwao. 

Katika safari yake hiyo ya masaa kadhaa nchini Iraq iliyolalamikiwa vikali na duru za kitaifa, kieneo na kimataifa siku ya Alkhamisi, Rais wa Marekani hakukutana na kiongozi yeyote wa serikali ya Baghdad.