Muhadhiri wa Chuo Kikuu China: Iran ndiye mshindi mbele ya Marekani
Muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Xiamen nchini China amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshinda katika kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.
Fan Khong Da, ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA ambapo akiashiria vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran amesema kuwa, mashinikizo ya Wamagharibi hususan Marekani dhidi ya Tehran sio jambo jipya kwani hata huko nyuma pia ni mambo yaliyoshuhudiwa. Amesisitiza kwamba huko nyuma pia Iran iliibuka mshindi mbele ya mashinikizo hayo ya Marekani.
Khong Da ameongeza kwamba, hii leo Iran haiwezi kuwaruhusu Wamagharibi waidhibiti nchi hiyo na sambamba na kukaribia kumbukumbu za miaka 40 ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, Iran inaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo na ustawi. Muhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Xiamen ameyazungumzia Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni tukio kubwa na muhimu duniani kote na kusema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapiga hatua za kujitegemea na uwezo mkubwa na kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yamepata mafanikio mengi mno ambayo yanashuhudiwa na watu wote.