Iran ni nchi yenye amani zaidi katika eneo
Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesema leo Iran ni nchi yenye amani zaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Meja Jenerali Bagheri ameyasema hayo leo mjini Tabriz Magharibi mwa Iran katika Kongamano la Kitaifa la Shahidi Hassan Bagheri Afshordi na kuongeza kuwa: "Watu wa Iran tokea mwanzo wa Mapinduzi ya Kiislamu wamekabiliana na vikwazo na njama za kuuangusha mfumo wa Kiislamu lakini si tu kuwa Mapinduzi ya Kiislamu hayakushindwa bali yanazidi kuimarika siku hadi siku."
Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hivi sasa Iran imebadilika na kuwa dola lenye nguvu kubwa katika eneo lakini kwamba pamoja na kuwa na nguvu hizo, inafuatulia mwenendo wa uadilifu na wala haina lengo la kuhujumu nchi yoyote.
Meja Jenerali Baqeri ameongeza kuwa iwapo Marekani na Israel zina nia chafu ya kuishambulia Iran, zinafahamu vyema kuwa zitapata jibu kali kutoka kwa taifa la Iran.
Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, leo majeshi ya Iran yana deni kubwa kwa Shahidi Hassan Baqeri kutokana na ustadi wake wa kivita. Amesema kati ya sifa za shahidi huyo katika zama za Kujihami Kutakatifu ni uono wake wa mbali wa kiintelijensia na utabiri wake wa masuala ya ulinzi; nukta ambazo zilipelekea adui agonge mwamba katika kukabiliana na majeshi ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran tokea mwaka 1980 hadi 1988.