Iran Inaongoza Mashariki ya Kati katika uga wa anga za mbali
Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (ISA) amesema: "Kutokana na jitihada za wasomi wake, Iran sasa inashika nafasi ya kwanza kieneo katika uga wa teknolojia ya anga za mbali na duniani inashika nafasi ya 11."
Mkurugenzi wa ISA Murtadha Barari ameongeza kuwa, katika kuunda satalaiti na pia katika kuunda chombo cha kurusha satalaiti na hali kadhalika katika ujenzi wa kituo cha kusimamia satalaiti, Iran imeweza kupata mafanikio makubwa sana. Aidha amesema Iran sasa ina uwezo wa kufuatilia harakati za satalaiti zake zote zilizo katika anga za mbali.
Mhandisi Barari amesisitiza kuwa, hivi sasa Iran ina vituo 30 vya utafiti katika uga wa anga za mbali na kwamba hivi sasa kuna idadi kubwa ya Wairani wanaopata mafunzo ya kitaalamu nchini ili kuendeleza sekta ya anga za mbali.
Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Iran pia imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama. Mafanikio haya ya Iran yanajiri pamoja na kuwepo vikwazo vya kila upande vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.