Iran: Hakuna mfungamano baina ya INSTEX na FATF
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51347-iran_hakuna_mfungamano_baina_ya_instex_na_fatf
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, ni jambo lisilokubalika kufungamanisha baina ya Mfumo wa Mabadilishano ya Kibiashara baina ya Ulaya na Iran (INSTEX) na taasisi kama ile ya FATF.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2019 04:37 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, ni jambo lisilokubalika kufungamanisha baina ya Mfumo wa Mabadilishano ya Kibiashara baina ya Ulaya na Iran (INSTEX) na taasisi kama ile ya FATF.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ikijibu misimamo ya nchi za Ulaya imesema kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kuanza kutekeleza Mfumo wa Mabadilishano ya Kibiashara (INSTEX) ambao umeanzishwa kwa kuchelewa na ukiwa na mapungufu kwa sababu utekelezaji wa majukumu ya nchi hizo wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA unaweza kuwa kigezo muhimu cha kupanga mahusiano yajayo ya nchi hizo na Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imezitaja tuhuma eti Iran inapanga na kufanya ugaidi barani Ulaya kuwa hazina msingi na kusisitiza kuwa: Iran ambayo yenyewe ni mhanga mkubwa wa mashambulizi ya kigaidi na nchi iliyo mstari wa mbele kupambana na makundi ya kigaidi kama Daesh, inatarajia kuwa nchi za Ulaya zitatupilia mbali sera zao za kindumakuwili kuhusiana na suala hilo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imesisitiza kuwa shughuli za kiulinzi za Iran ni kwa ajili ya kujihami na kusema kuwa: Iran kamwe haitafanya mazungumzo na nchi yoyote nyingine kuhusiana na suala hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imelaani sera za kutumia haki za binadamu kama wenzo wa kisiasa dhidi ya nchi zinazojitawala na kusema kuwa: Misimamo ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na Iran haiwezi kukubalika katika eneo ambako tatizo na mgogoro wake mkubwa zaidi ni utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai zinazofanywa na utawala wa Saudi Arabia. 

Itakumbukwa kuwa, jioni ya jana Jumatatu Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa iliyopinga maamuzi ya Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA lakini wakati huo huo imekariri madai ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.