Zarif: Amani haiwezi kupatikana kwa kutumia sera za mabavu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa fikra zinazotokana na mitazamo ya kibeberu na utumiaji wa silaha zenye uharibifu zinapaswa kubadilishwa na kuwa fikra ya mazungumzo na maelewano.
Dakta Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo leo katika Kongomano la Kimataifa la Nowrouz linalofanyika mjini Tehran. Ameongeza kuwa, sisi sote tunapaswa kutumia lugha ya Iran, lugha ya ardhi ya Nowrouz na utamaduni wa Nowrouz kutangaza waziwazi kwamba, haiwezekani kutengeneza amani kwa kutumia mabavu na tunapaswa kutumia mienendo na fikra za Kinowrouzi ili kuionesha dunia kwamba, kipindi cha ubeberu kimepita na kuyoyoma.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Wale waliotumia dola trilioni 7 katika eneo la Mashariki ya Kati hali yao hii leo ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma na wanapaswa kuelewa kuwa, hali hiyo itaendela kuwa hivyo hivyo hata kama watatumia dola trilioni 70 au trilioni 700. Amesisitiza kuwa, madola hayo hayawezi kupata amani hadi pale yatakapokubali kwamba, wanadamu wana mustakbali na matatizo ya pamoja na njia ya utatuzi ya pamoja.
Itakumbukwa kuwa Disemba mwaka jana na baada ya kupata pigo katika Umoja wa Mataifa, Rais Donald Trump wa Marekani alisema nchi hiyo imetumia kijinga dola trillioni saba Mashariki ya Kati.
Kongamano na sherehe ya kimataifa ya Nowrouz inafanyika kwa ushirikiano wa Iran na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).