Nguvu za Marekani zinazidi kudidimia na kudhoofika
Admeri Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nguvu ya Marekani imo katika hali ya kudhoofika.
Shamkhani aliyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika Kongamano la Kitaifa la Historia Simulizi ya Kujihami Kutakatifu mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Marekani, madola ya Magharibi na tawala vibaraka katika eneo zimetumia magaidi na mamluki kwa lengo la kuangamiza harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu lakini, vijana wanamuqawama, Jeshi la Syria, Harakati ya Hashd al Shaabi ya Iraq na Ansarullah ya Yemen, pamoja na Walinzi wa Haram Takatifu wamethibitisha kuwa, nchi za Magharibi si mhimili wa dunia na wamesambaratisha dhana potofu iliyokuwa imejengeka kuhusu nguvu za Marekani."
Leo katika hali ambayo eneo linashuhudia kusambaratishwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh huku harakati ya muqawama ikipata nguvu, Marekani sasa iko mbioni kupotosha fikra za walimegnu kutoka maudhui asili ambayo ni kufeli sera zake na za Israel katika eneo.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni kitovu cha fitina na vita katika eneo, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, umeshiriki katika vita muhimu na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina na kushindwa katika vita vyote hivyo. Katika vita vya siku 33, siku 22, na siku nane, wapiganaji wa harakati za Muqawama, ambao ikilignaishwa na Israel hawakuwa na zana za kutosha za kivita, waliweza kupata ushindi. Ushindi huo ulikamilika katika vita vya siku 51 vya Ghaza. Kushindwa mara kadhaa utawala haramu wa Israel katika mapambano na harakati za muqawama nchini Lebanon na Ghaza ni jambo ambalo linaonyesha kuwa Israel, na muungaji mkono wake mkuu yaani Marekani wamedhoofika kwa kiasi kikubwa.
Katika tathmini yake kuhusu matokeo ya ushindi huo wa muqawama, Shamkhani amesema: "Leo pamoja na kuwa gharama kubwa imetumika kwa ajili ya kuidhaminia usalama Israel, tunashuhudia kugonga mwamba stratijia za Marekani na tawala vibaraka katika eneo katika kudhamini usalama wa mipaka ya utawala wa Israel. Utawala ghasibu wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu ungali unahisi hatari hata ndani ya mipaka yake."
Katika hali kama hii, Marekani, Israel, Saudi Arabia na baadhi ya tawala fisadi na haramu katika eneo, kwa kuunga mkono magaidi wa ISIS zilihatarisha usalama wa Iraq na Syria hata kufikia kiwango cha kuwepo hatari ya kusambaratika nchi hizo; lakini hazikufanikiwa na zilishindwa mbele ya wanamuqawama.
Mapambano na ushindi wa wanamuqawama una tathmini mbili, awali ni kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni si ndoto tena bali ni jambo ambalo sasa ni ukweli wa mambo na pili na muhimu zaidi ni kuwa nguvu za Marekani ziko katika muelekeo wa kudhoofika na kudidimia katika eneo.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika hotuba yake hivi karibuni alipokutana na maelfu ya watu kutoka mkoa wa Azerbaijan Mashariki aliashiria kudhoofika mrengo wa uistikbari wa Kimataifa ambao kinara wake ni Marekani na kusema: "Kuna dalili nyingi zinazoonyesha kuwa, nguvu na uwezo wa Marekani duniani unazidi kudidimia na Marekani leo ni dhaifu zaidi ya ilivyokuwa miongo minne iliyopita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alibainisha zaidi kwa kusema: "Watawala wenye akili finyu wa Marekani walizialika baadhi ya nchi washirika wake na madola dhaifu na yenye woga katika mkutano wa Warsaw kwa ajili ya kuchukua uamuzi dhidi ya Iran, lakini mkutano huo umefeli na haujakuwa na natija yoyote, na haya yote ni ishara ya udhaifu."
Mtazamo huu ndio alioubainisha Admeri Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliposema: "Nguvu za Marekani zinazidi kudhoofika duniani na huu ni ukweli wa mambo."
Kuushindwa Marekani kuleta mabadiliko ya kistratijia katika eneo na kushindwa njama za kuunda muungano dhidi ya Iran na kufeli makumi ya njama nyiginezo ni nukta zinazoashiria kufeli matarajio ya Marekani na waitifaki wake.