Mwaka mpya katika matazamio ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, ametoa ujumbe maalumu kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1398 Hijria Shamsia, na kuupa mwaka huo mpya jina la mwaka wa "Kustawi Uzalishaji."
Katika kuutathmini mwaka uliomalizika wa 97, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameuelezea mwaka huo kuwa ni mwaka uliokuwa na matukio mengi na akafafanua kwa kusema: "Katika mwaka huo, adui alipanga njama nyingi dhidi ya Iran, lakini taifa la Iran, liliweza kung'aa kwa maana halisi ya neno hilo na hivyo, kwa nguvu, uono wa mbali na hima ya vijana, njama hizo zimesambaratishwa."
Taifa kubwa la Iran, leo limeuanza mwaka mpya katika hali ambayo, katika mwaka uliopita wa 97 liliwathibitishia maadui kwa uwezo na nguvu kamili, kuwa haliwezi kushindika; na kwa mshikamano wa watu wake likasimama imara kukabiliana na njama za Marekani na mashinikizo ya Ulaya na kuonyesha kwamba, kwa kushikamana na misingi na malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, inawezekana kukabiliana nao na kuupa changamoto kali ubeberu wa madola makubwa ya dunia.
Katika kubainisha umuhimu wa harakati hiyo adhimu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jibu na radiamali ya wananchi wa Iran kwa vikwazo vikali vya Marekani na Ulaya katika nyuga za kisiasa na kiuchumi, lilikuwa imara na madhubuti, na akaongezea kwa kusema: "Katika uga wa kisiasa, dhihirisho la wazi la jibu hilo ni maandamano makubwa ya 22 Bahman (11 Februari) na misimamo ya wananchi katika kipindi chote cha mwaka. Katika uga wa makabiliano ya kiuchumi pia, taifa la Iran limeweza "kuongeza ubunifu wa kisayansi na kiufundi", "kuimarisha kwa kiwango kikubwa mashirika ambayo msingi wake ni elimu", kuimarisha uundwaji wa miundo msingi ya ndani ya nchi kama vile kufunguliwa awamu kadhaa za vituo vikubwa vya uzalishaji gesi asilia kusini mwa nchi na kufunguliwa kituo kikubwa cha usafishaji mafuta cha Bandar Abbas. Na kwa kufanya hivyo, taifa la Iran limeweza kuonyesha nguvu, haiba na adhama yake mbele ya uadui na uhabithi wa maadui na kuzidisha heshima ya taifa, mapinduzi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu."
Katika ujumbe wake wa mwaka mpya, Ayatullah Khamenei, ameashiria nukta muhimu ambazo kwa kweli ndizo zinazojenga mhimili mkuu na msingi wa izza na nguvu za taifa la Iran.
Uthabiti na ungangari ulioonyeshwa na taifa la Iran katika kuyakabili mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani na Ulaya ni miongoni mwa masuala hayo muhimu, ambalo lilifanikishwa katika mwaka uliopita kwa kukipita kipindi kigumu na cha misukosuko. Hata hivyo kwa kudumisha umoja na mshikamano, taifa la Iran lilikivuka kipindi hicho kwa heshima na mafanikio. Uthabiti huo ulionyesha kwamba, licha ya kukabiliwa na dhiki na tabu za kiuchumi, wananchi wa Iran katu hawatasalimu amri mbele ya watumiaji mabavu.
Suala jengine muhimu lililoashiriwa katika ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kung'ara taifa la Iran katika uga wa utumiaji uwezo na vipawa vya ndani katika sekta mbali mbali za uchumi na uzalishaji elimu. Harakati hiyo imekuwa na umuhimu wa kistratejia na taathira kubwa katika kupunguza mbinyo wa vikwazo.
Kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi wananchi walivyoipokea kaulimbiu ya mwaka 97 ya "kuunga mkono bidhaa za Kiirani" na athari chanya za hatua hiyo na akaeleza kwamba: "Mwaka huu, suala la kimsingi ni " Uzalishaji", kwani iwapo uzalishaji utakuwepo, matatizo ya kimaisha na ajira yataweza kutatuliwa na pia nchi haitakuwa tegemezi kwa maajinabi na maadui; na hata jambo hilo linaweza kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la thamani ya sarafu ya taifa. Kwa msingi huo, nimeitangaza kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni "Kustawi Uzalishaji".
Tajiriba ya mwaka uliopita na matukio ya misukosuko na mafanikio yaliyoshuhudiwa katika nyuga za kisiasa na kiuchumi imeonyesha kuwa, moja ya malengo makuu ya maadui ni kujenga hali ya kukatisha tamaa, kupoteza matumaini na kuhisi nchi imefikia kwenye mkwamo katika nyuga za kisiasa na kiuchumi kwa kuyadogesha au kuyakana matunda na mafanikio yasiyo na mbdala uliyopata mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Katika suala hilo, kujaribu kujenga dhana ndani ya jamii ya kuwepo matatizo makubwa na mengi zaidi ni moja ya malengo yaliyofuatiliwa na Marekani katika vita vya kisaikolojia na kipropganda ilivyoendesha dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa kuzingatia hali hiyo, ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi na hatua yake ya kuichagua kaulimbiu ya "Kustawi Uzalishaji", vinatoa matazamio na mwanga wa wazi wa matumaini kwa taifa la Iran na jinsi taifa hili litakavyoweza kuonyesha nguvu, haiba na adhama yake sambamba na kuwa thabiti na ngangari katika kukabiliana na uadui na uhabithi wa maadui.../