Rais Rouhani: Serikali itafidia hasara walizopata waathiriwa wa mafuriko
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52439
Rais Hassan Rouhani amesema: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu itahakikisha kwa suhula zote ilizonazo na kwa uwezo wake wote inafidia hasara walizopata watu wote walioathiriwa na mafuriko.
(last modified 2025-07-16T10:13:10+00:00 )
Mar 27, 2019 16:10 UTC
  • Rais Rouhani: Serikali itafidia hasara walizopata waathiriwa wa mafuriko

Rais Hassan Rouhani amesema: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu itahakikisha kwa suhula zote ilizonazo na kwa uwezo wake wote inafidia hasara walizopata watu wote walioathiriwa na mafuriko.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao cha baraza la mawaziri, ambapo sambamba na kueleza masikitiko aliyonayo kutokana na maafa yaliyowapata wananchi kutokana na mafuriko yaliyotokea katika baadhi ya mikoa nchini, amesema: Hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita hadi sasa zimekuwa na athari nzuri lakini hazitoshi, na inapasa hatua zaidi zichukuliwe katika uwanja huo.

Rais Rouhani amesema, uzoaji taka chini ya mito, kuandaa mkakati mpana wa kuilinda miji inayokabiiwa na hatari ya mafuriko, kuyasomba maji kuelekea vyanzo vya maji na mito mikuu, kujenga vizuizi vya maji na kuangalia upya usanifu wa barabara na njia za reli ni miongoni mwa hatua za lazima zinazopasa kuchukuliwa ili kubadilisha vitisho vilivyopo vya mafuriko kuwa ni fursa.

Hali ya mafuriko iliyokumba baadhi ya mikoa ya Iran

Kufuatia mvua kali zilizonyesha hivi karibuni ambazo hazijawahi kushuhudiwa, mikoa kadhaa ya Iran ikiwemo ya Golestan, Mazandaran, Fars na Lorestan imekumbwa na gharika na mafuriko. 

Watu 21 wamefariki dunia na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika mafuriko ya siku ya Jumatatu yaliyotokea katika mji wa Shiraz, kusini mwa Iran.../