Waziri Mkuu wa Pakistan awasili Iran kwa ziara rasmi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52996-waziri_mkuu_wa_pakistan_awasili_iran_kwa_ziara_rasmi
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan leo Jumapili amewasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran na kulakiwa rasmi na mkuu wa mkoa pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa mkoa wa Khurassan Razavi.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 21, 2019 09:30 UTC
  • Waziri Mkuu wa Pakistan awasili Iran kwa ziara rasmi

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan leo Jumapili amewasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran na kulakiwa rasmi na mkuu wa mkoa pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa mkoa wa Khurassan Razavi.

Alipowasili alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Khurassan Razavi Ali Reza Razm Hosseini kabla ya kufanya ziara katika Haram takatifu ya Imam Ridha AS, Imam wa Nane wa Mashia mjini Mashhad. 

Ziara hiyo imefanyika tarehe 15 Shaabab ambapo Waislamu wa madhehebu ya Shia  wanaadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Mahdi, Imam wa 12 wa Mashia.

Waziri Mkuu wa Pakistan anaitembelea Iran kufuatia mwaliko rasmi wa Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Waziri Mkuu wa Pakisitan amewasili Tehran leo usiku na anatazamiwa kulakiwa rasmi Jumatatu asubuhi.

Safari ya Imran Khan nchini Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kustawisha uhusiano wa nchi hizi mbili jirani hasa ushirikiano wa kieneo katika kupambana na ugaidi na kuiamrisha usalama mipakani. 

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan baada ya kuwasili mjini Mashhad, Aprili 21 2019

Imran Khan amesema nchi yake inalipa umuhimu mkubwa suala la uhusiano wake na Iran na kuongeza kuwa analenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili jirani katika safari yake tarajiwa mjini Tehran.

Alitoa tamko hilo Alhamisi wakati alipokutana na Balozi wa Iran mjini Islamabad Mahdi Honardoost ambapo pande mbili zilijadili safari hiyo.

Imran Khan ambaye alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan kufuatia ushindi wa chama chake katika uchaguzi mkuu wa Julai 2018 ametangaza kuwa tayari kuwa mpatanishi wa mgogoro uliopo katika uhusiano wa Iran na Saudi Arabia. Mwezi Oktoba mwaka jana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman alitembelea Pakistan.