May 27, 2019 04:27 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran akosoa njama za Wamagharibi dhidi ya Wapalestina

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amekosoa vikali njama za nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zilizopewa jina la 'Muamala wa Karne' dhidi ya Wapalestina, huku akitoa mwito wa mahudhurio makubwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

Ali Larijani alitoa mwito huo jana Jumapili katika kikao cha wazi cha Bunge hapa Tehran na kufafanua kuwa, "Lengo la mpango huo eti wa amani ya Wapalestina ni kutaka kuyeyusha na kutokomeza kikamilifu kadhia ya Palestina."
Dakta Larijani ameutaja mpango huo wa Marekani dhidi ya Wapaletina kama njama hatari, isiyo ya kutegemewa, ya kihaini na isiyo ya kiutu."

Spika wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa, njama kubwa ya Wamaghairibi dhidi ya Marekani inapikwa hivi sasa katika eneo, huku akitoa mwito kwa nchi zenye kupenda haki kususia kongamano la biashara la Bahrain, ambalo litakuwa jukwaa ya kuzinduliwa mpango huo wa Marekani dhidi ya Wapalestina.

Mpango wa 'Muamala wa Karne' utazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' litakalofanyika mjini Manama Juni 25 na 26.

Maandamano ya Siku ya Quds mjini Tehran mwaka jana 2018

Wapalestina wamewataka Waislamu kote duniani kusimama kidete dhidi ya njama hizo batili za Marekani zilizopewa anwani ya "Muamala wa Karne".

Spika wa Bunge la Iran amewataka Waislamu na wapenda haki kote dunia kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Tags