Iran kuongeza mara 4 urutubishaji wa urani, kupitisha kiwango cha kilo 300
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54180
Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanzia Juni 27 itapitisha kiwango cha urutubishaji wa urani mara nne zaidi, na kwamba akiba yake ya urani itapita kiwango cha kilo 300 kilichoanishwa kwenye makubaliano ya nyuklia kufikia tarehe hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 17, 2019 12:42 UTC
  • Iran kuongeza mara 4 urutubishaji wa urani, kupitisha kiwango cha kilo 300

Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanzia Juni 27 itapitisha kiwango cha urutubishaji wa urani mara nne zaidi, na kwamba akiba yake ya urani itapita kiwango cha kilo 300 kilichoanishwa kwenye makubaliano ya nyuklia kufikia tarehe hiyo.

Behrouz Kamalvandi amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari katika kituo cha maji mazito cha Arak na kubainisha kuwa, "Hii leo, safari ya kupitisha kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa imeng'oa nanga, na ndani ya siku 10, tutapitisha kiwango hicho."

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ilikubali kwa khiari kujiwekea mipaka na vizingiti katika mradi wake wa nyuklia wenye malengo ya amani, lakini hivi sasa imeamua kungalia upya mipaka hiyo.

Mwezi uliopita, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran alisema Tehran hailazimiki tena kuchunga kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa kwa asilimia 3.67 na vile vile kiwango cha tani 130 za maji mazito ya nyuklia.

Dk Ali Akbar Salehi alisema hayo na kufafanua kuwa, uamuzi huo wa Iran wa kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA unaendana na kifungu nambari 26 cha mapatano hayo.

Kituo cha maji mazito cha Arak

Kwa mujibu wa kifungu hicho, kila pale ambapo Iran itahisi kuwa upande wa pili haukutekeleza ahadi zake, Tehran nayo inaweza kupunguza uwajibikaji wake kwa baadhi ya ahadi za JCPOA ili kuufanya upande wa pili uangalie upya msimamo wake.

Tayari  Iran imezifahamisha rasmi nchi tano (4+1) zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kuhusiana na uamuzi wake wa kusimamisha kwa muda utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake kuhusu mapatano hayo, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa.