Polisi wa Iran auawa shahidi akipambana na magenge ya mihadarati
Afisa mmoja wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameuawa shahidi wakati akipambana na magenge ya madawa ya kulevya katika eneo la Minab, mkoani Hormozgan, kusini mwa Iran.
Tukio hilo lilitokea Jumanne usiku katika eneo la kilomita 30 la barabara kuu ya Minab kuelekea Bandar Abbas. Afisa huyo wa Jeshi la Polisi la Iran alijeruhiwa na wafanya magendo wa madawa ya kulevya na kufa shahidi hospitalini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mtari wa mbele katika vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya duniani. Hadi hivi sasa karibu maafisa wake elfu nne wameshauawa shahidi kwenye vita hivyo na wengine wengi wamejeruhiwa.
Umoja wa Mataifa umeipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake za kupambana na mihadarati ambayo sehemu yake kubwa huelekea katika nchi za Ulaya na Marekani. Umoja wa Mataifa umesema, Iran ni mbeba bendera ya vita dhidi ya madawa ya kulevya duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, asilimia 75 ya madawa ya kulevya ya Tiryak, asilimia 61 ya mihadarati ya morphine na asilimia 17 ya madawa ya kulevya ya heroine duniani yamegunduliwa na kukamatwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.