Rouhani na al Abadi wajadili mapambano dhidi ya ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa Iraq wamefanya mazungumzo ya simu wakijadili hali ya sasa ya Mashariki ya Kati husuan mipango ya serikali ya Iraq ya kurejesha amani nchini humo na kupambana na ugaidi.
Rais Hassan Rouhani amesema katika mazungumzo hayo kwamba, kupambana na makundi ya kigaidi hususan lile la Daesh ni wadhifa wa nchi zote zinazowajibika diniani na kuongeza kuwa, Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na serikali na wananchi wa Iraq katika kupambana na makundi hayo.
Rais Rouhani amempongeza Waziri Mkuu wa Iraq kutokana na ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya makundi ya kigaidi na kusema: Jamhuri ya Kiislamu inatambua amani na usalama wa Iraq kuwa ni amani na usalama wake na itafanya jitihad zote kuimarisha usalama nchini Iraq.
Rais Hassan Rouhani pia amezitaka nchi mbalimbali kuacha nara tupi na kuingia katika awamu ya vitendo katika suala la kupambana na ugaidi na kusema: Inasikitisha kwamba baadhi ya nchi zinazodai kupambana na ugaidi zingalia zinatoa misaada ya silaha na kununua mafuta kutoka kwa kundi la kigaidi la Daesh.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh ni tishio kwa eneo la Mashariki ya Kati na maeneo mengine ya dunia na kusema, taifa na serikali ya Iraq inapongeza msimamo imara wa Iran katika kupambana na Daesh. Vilevile amesisitiza udharura wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa pande hizo mbili.