Brigedia Jenerali Nilforooshan: Israel imezungukwa na Iran kila upande
Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umezingirwa kila upande na Iran na kuuonya utawala huo haramu dhidi ya kuchukua hatua yoyote ya kichokozi dhidi ya taifa hili.
Brigedia Jenerali Abbas Nilforooshan ambaye ni Naibu Kamanda wa Operesheni za SEPAH amesema utawala haramu wa Israel ni dhaifu mno na hauwezi kuwa tishio kwa taifa kubwa la Iran. Ameeleza bayana kuwa, "Taifa lenye nguvu la Iran limeuzingira utawala dhaifu wa Israel upande wa mashariki, magharibi, kusini na kaskazini na kwa msingi huo, utakuwa unajisainia waranti wa kifo iwapo utathubutu kuiletea chokochoko Iran."
Amesema utawala huo batili unatapatapa na unajaribu kuchukua hatua za kujikwamua kwenye kinamasi katika hali ambayo, hivi sasa ni wazi zaidi kuwa utawala huo upo katika pumzi zake za mwisho.
Brigedia Jenerali Abbas Nilforooshan ametahadharisha kuwa, "iwapo watawala wa Tel Aviv watafanya kosa dogo la kuishambulia Iran, basi taifa hili litausambaratisha utawala huo na kumwaga mabaki yake kwenye Bahari ya Mediterranean."
Kamanda huyo wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, migogoro na mpasuko mkubwa unaoshuhudiwa hivi sasa ndani ya utawala huo haramu katika nyuga za kijamii, kisiasa na kiutamaduni ni mkubwa kiasi kwamba, iwapo Tel Aviv itajiingiza kwenye kinamasi cha vita, basi itaisogeza zaidi Israel katika ncha ya kuporomoka.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina azma wala haja ya kuingia vitani, lakini imejiandaa kikamilifu kukabiliana na chochoko zozote za maadui.