IRGC yatibua njama ya Waarabu na Wazayuni ya kumuua Jenerali Soleimani
Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Iran kimetibua njama za nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel za kumuua Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH, Meja Jenerali Qassem Soleimani.
Hossein Taeb, Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la SEPAH amesema njama hizo zilikuwa zimepikwa na taasisi za kijasusi za Wayahudi na Waarabu na kwamba mauaji hayo yalipangwa kufanyika kati ya Septemba 8 na 9 mwaka huu.
Amesema taasisi za kijasusi za Wayahudi na Waarabu zilikisajili kikundi cha kigaidi ambacho kilitazamiwa kujipenyeza Iran na kufanya mauaji hayo katika mkoa wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran.
Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la SEPAH amefafanua kuwa, "Magaidi hao walipaswa kukodisha nyumba karibu na Husseiniyya ya babake Jenerali Soleimani ambaye ni marehemu, na kutega ardhini mada za milipuko za kilo 350 hadi 500, wakati wa matembezi ya Maombolezo ya Tasu'a na Ashura ambayo Jenerali Soleimani alishiriki.
Amesema kufuatia operesheni ya hali ya juu ya Kitengo cha Intelijensia cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Iran, njama hizo ziliweza kutibuliwa kabla ya kutekelezwa.
Wanachama watatu wa kikundu hicho cha kigaidi walitiwa mbaroni, na baadaye wakakiri kuwa njama hizo zilikuwa zimepangwa kwa miaka kadhaa na taasisi za kijasusi za Mayahudi na Waarabu.