Mwanasayansi wa Iran anashikiliwa Marekani kinyume cha sheria
Mwanasayansi Muirani, Profesa Masoud Suleimani, anashikiliwa nchini Marekani kwa muda wa mwaka mmoja sasa kinyume cha sheria.
Mnamo Oktoba 25, 2018, Profesa Suleimani ambaye ni mwanasayansi wa seli shina na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Tarbiat Modares, alifika katika uwanja wa ndege wa Chicago kufuatia mwaliko wa taasisi moja ya utafiti Marekani. Punde baada ya kuwasili Profesa Suleimani alitiwa mbaroni an makachero wa FBI na tokea wakati huo hadi sasa yuko kizuizini bila mawasiliano yoyote na jamaa zake.
Kliniki ya Mayo ya Minnesota ilikuwa imemualika Profesa Suleimani kwa ajili ya utafiti kuhusu wagonjwa wa kiharusi.
Waendesha mashtaka huko Atlanta wanamtuhumu Suleimani kuwa eti alikuwa anapanga kuchukua kutoka Marekani mada ya kibiolojia na kuzileta Iran kinyume cha sheria za vikwazo dhidi ya Iran kwa kushirikiana na wanafunzi wake wawili ambao wana uraia wa Marekani. Profesa Suleimani ana matatizo kadhaa ya kiafya ambayo yamezidi kuwa mabaya akiwa kizuizini.
Aidha mama yake mzazi amefariki wakati Suleimani akiwa anashikiliwa Marekani na hadi sasa hajafahamishwa kuhusu tukio hilo.
Wanaharakati wa kijamii wameanzisha kampeni ya kimataifa ya kutaka Profesa Suleimani aachiliwe huru. Kampeni hiyo ya kimatiafa inayojulikana kama #Free_Masoud_Soleimani inalenga kuwahimiza wakuu wa Marekani wamuachilie huru.