Larijani: Iran imeandaa mazingira kwa ajili ya Afrika Kusini kuwekeza nchini
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mchakato wa kuandaa mazingira kwa ajili ya Afrika Kusini kuwekeza hapa nchini umekamilika na kusisitiza kwamba, uhusiano wa pande mbili unahitaji kupigwa jeki katika ushirikiano wa kiuchumi.
Ali Larijani amesema hayo katika mazungumzo yake na Vika Mazwi Khumalo, Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran na kusisitiza kuwa, kutokana na ukweli kwamba Afrika Kusini ni nchi muhimu sana barani Afrika, kuna umuhimu kwa taifa hilo kuwa muasisi wa kuwa na uhusiano wa kibiashara na Iran.
Kadhalika sambamba na kusisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga za Bunge na siasa, Dakta Larijani ameeleza bayana kuwa, kuna udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kiufundi na kisayansi wa nchi hizi mbili kwa kushirikisha sekta za serikali na za watu binafsi.
Kwa upande wake, Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran sambamba na kusifu uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi yake na Iran, amesisitizia udharura wa kustawisha ushirikiano wa pande zote baina ya nchi hizi katika nyuga mbalimbali.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuonana na Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini hapa Tehran ambapo alitilia mkazo pia udharura wa kustawisha ushirikiano wa pande zote baina ya nchi mbili akisisitiza kuwa, kustawishwa uhusiano huo ni kwa manufaa ya nchi zote mbili na maeneo yao.
Pande hizo mbili pia zilisaini hati za ushirikiano wa kimataifa na kusisitiza udharura wa kudumishwa ushirikiano wa nchi mbili kupitia Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), kupambana na ugaidi na kendelezwa mashauriano na jitihada za kidiplomasia za kuimarisha amani na usalama duniani.