Maombolezo ya Imam Ali Ridha (as) nchini Iran
Leo Jumanne tarehe 30 Swafar 1441 Hijiria sawa na tarehe 29 Oktoba Miladia inasadifiana na siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Ali ar-Ridha (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) miaka 1237 iliyopita.
Kwa mnasaba huo, nchi nzima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea jana usiku imezama katika maombolezo ya kumkumbuka mtukufu huyo, na hasa katika mji mtakatifu alikozikwa wa Mash'had, kaskzini mashariki mwa nchi.
Barabara zote zinazoelekea katika Haram ya Imam Ridha (as), Imam wa nane wa Waislamu wa Kishia, katika mji huo zimejaa umati wa waombolezaji waliovalia mavazi meusi na waliofika huko kutoka pembe zote za nchi na maeneo mengine ya dunia kwa ajili ya kuomboleza kifo cha mtukufu huyo wa Nyumba ya Mtume (saw).
Imam Ridha (as) alizaliwa katika mji wa Madina nchini Saudi Arabia mwaka 148 Hijiria na kuuawa shahidi katika siku ya mwisho ya mwezi wa Swafar mwaka 203 Hijiria.
Imam Ridha (as) aliishi katika kipindi ambacho watu walikuwa na hamu kubwa ya kuwajua Watu wa Nyumba ya Mtume na kizazi chake kitoharifu (as) na kuimarika nafasi yao miongoni mwa watu.
Kwa kuhisi hatari kutokana na mapenzi na uungaji mkono huo mkubwa wa watu kwa Ahlul Bait wa Mtume (saw) Ma'mun, mtawala wa Bani Abbas katika kipindi hicho, alipanga njama ya kumpa sumu na kumuua Imam (as).
Katika usiku wa kuamkia siku ya kuuawa shahidi Imam Ridha (as), watu wa Iran hukusanyika misikitini na katika maeneo mengine ya ibada na marasimu ya kidini, na hasa katika kaburi lake huko Mash'had, kwa madhumini ya kutoa heshima zao na kumuomboleza mtukufu huyo, mjukuu wa Mtume (saw).