SEPAH: Watu milioni 8.5 wameuawa kutokana na uingiliaji mambo wa Marekani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema watu zaidi ya milioni nane na laki tano wameuawa kutokana na uingiliaji wa mambo wa Marekani wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja katika eneo na katika ulimwengu wa Kiislamu, ndani ya miaka 40 iliyopita.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa SEPAH ameyasema hayo leo Jumamosi na kufafanua kuwa, "Marekani ndiye muuzaji mkubwa wa silaha duniani na mhusika wa vita vingi vilivyoshuhudiwa na vinavyoendelea kushuhudiwa katika kona mbalimbali za duniani. Uwezo wa kijeshi wa Marekani umeonesha kuwa Washington haitaki jingine ghairi ya kuivuruga dunia."
Jenerali Salami amesema haiingii akilini kujiita kuwa mbeba bendera ya demokrasia duniani kwa upande mmoja, huku ukipanga mapinduzi katika nchi mbalimbali kwa upande mwingine.
Amebainisha kuwa, katika hali ambayo Marekani inadai kuwa inapambana vikali na silaha za maangamizi, lakini nchi hiyo hiyo ndiyo ya kwanza kuunda na kutumia silaha za atomiki.
Kamanda Mkuu wa SEPAH ameashiria madai ya Marekani kuwa ni mtetezi nambari moja wa haki za binadamu na mpambanaji wa ugaidi, katika hali ambayo (Rais Donald) Trump binafsi amewahi kukiri kuwa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) liliundwa na Washington wakati wa utawala wa mtangulizi wake Barack Obama.
Meja Jenerali Hussein Salami ameongeza kuwa, kadri Marekani inavyogharamika ili liwe taifa lenye nguvu kubwa zaidi duniani, ndivyo inavyozidi kufeli na kupata hasara.