Apr 24, 2016 16:59 UTC
  • Iran yasisitiza kuimarisha uhusiano na Afrika Kusini

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema watu wa Iran walisimama bega kwa bega na kuwaunga mkono wazalendo wa Afrika Kusini wakati wakipambana na utawala wa makaburuwabaguzi wa rangi.

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari akiwa ameandamana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini. Rais Rouhani ameitaja safari ya Zuma kuwa muhimu sana na kuongeza kuwa: "Katika safari ya Jacob Zuma Tehran, kutaimarishwa uhusiano wa nchi mbili muhimu yaani Iran kama nchi yenye taathira katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati na Afrika Kusini kama nchi muhimu barani Afrika."

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, tokea ishike madaraka serikali ya chama cha ANC Afrika Kusini baada ya kuangushwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na Afrika Kusini.

Rouhani ameongeza kuwa katika mazungumzo ya faragha na ya wazi na Jacob Zuma, pande mbili zimejadili kuhusu kutumia uwezo wa Iran na Afrika Kusini katika uga wa uchumi, biashara, sayansi, teknolojia na pia kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.

Rais wa Iran pia amesema Iran na Afrika Kusini zinaweza kuimarisha uhusiano katika sekta za benki ili kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Katika mkutano huo wa leo wa marais wa Iran na Afrika Kusini, nchi mbili zimetiliana saini mikataba nane kuhusu kuimarisha uhusiano katika sekta mbali mbali. Zuma aliwasili Tehran leo Jumapili akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi unaojumuisha watu 180 kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Tags