Jumuiya ya Kiislamu yasisitizia umoja na kuwa macho Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57315-jumuiya_ya_kiislamu_yasisitizia_umoja_na_kuwa_macho_waislamu
Viongozi wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani walioshiriki mkutano wa 12 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu hapa Tehran wamesisitizia udharura wa kudumishwa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu kote duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 17, 2019 04:05 UTC
  • Jumuiya ya Kiislamu yasisitizia umoja na kuwa macho Waislamu

Viongozi wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali duniani walioshiriki mkutano wa 12 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu hapa Tehran wamesisitizia udharura wa kudumishwa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu kote duniani.

Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi baada ya kumalizika mkutano huo wa siku moja imesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina ndio maudhui kuu na muhimu zaidi hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na suala hilo linapaswa kupewa uzito na kuzingatiwa katika kila ngazi.

Aidha taarifa hiyo imesisitiza juu ya udharura wa ulimwengu wa Kiislamu kuwa macho na kusimama kidete dhidi ya njama za maadui. Taarifa hiyo imesema: "Maadui wa Uislamu haswa Marekani na utawala wa Kizayuni wanataka kutawala na kudhibiti ulimwengu wa Kiislamu ili wapore rasilimali zao." 

Taarifa ya washiriki wa mkutano wa 12 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu hapa Tehran imewataka Waislamu kushikamana na mafundisho ya Qurani na sunna za Mtume Mtukufu SAW na kusisitiza kwamba umoja wao ndio silaha ya kuzishinda njama za maadui.

Washiriki wa mkutano wa 12 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu 

Akizungumza katika mkutano huo hapa Tehran, Ali Akbar Velayati, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu ambaye pia ni mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, ubeberu wa kimataifa ukingozwa na Marekani, unafanya njama za kuzuia ongezeko la wafuasi wa Uislamu linalozidi kila uchao.

Mkutano huo wa 12 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu umemalizika sambamba na kumalizika Kongamano la 33 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu hapa nchini Iran.