Meja Jenerali Mousavi: Iran itatoa jibu kali na la haraka ikichokozwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58271-meja_jenerali_mousavi_iran_itatoa_jibu_kali_na_la_haraka_ikichokozwa
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikosi vya Jeshi la Iran viko tayari kutoa jibu kali na la haraka kwa aina yoyote ya vitisho na chokochoko za adui.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2020 23:22 UTC
  • Meja Jenerali Mousavi: Iran itatoa jibu kali na la haraka ikichokozwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikosi vya Jeshi la Iran viko tayari kutoa jibu kali na la haraka kwa aina yoyote ya vitisho na chokochoko za adui.

Meja Jenerali Sayyid Abdulrahim Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mazoezi ya kijeshi ambayo yalifanyika katika mkoa wa Fars, kusini mwa nchi na kuongeza kuwa, "Kikosi cha Nchi Kavu kimejiandaa kikalimifu kulinda mipaka yote ya taifa hili iwapo maadui watajaribu kujipenyeza nchini."

Meja Jenerali Mousavi ameongeza kuwa ujumbe wa mazoezi hayo kwa maadui ni kuwa, iwapo wanapanga njama, basi wafahamu kuwa vikosi vya Iran viko tayari kabisa kutoa pigo kwa uchokozi wa maadui na kuwa vitaendelea kusimama kidete na kwa nguvu kubwa zaidi.

Mazoezi ya kijeshi mkoani Fars

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa vikosi vya Jeshi la Iran viko katika kilele cha utayarifu na vitatekeleza amri yoyote kwa kasi ya juu kabisa.

Amesema silaha na zana za kijeshi za Iran zimeundwa na wataalamu wa hapa hapa nchini na kwamba, "Baadhi ya zana za kijeshi zilizotumiwa kwenye maneva ya kijeshi mkoani Fars zinadhihirisha wazi uwezo mkubwa wa kujihami taifa hili."