Wairani waandamana kote nchini kuomboleza mauaji ya Jen. Soleimani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58286-wairani_waandamana_kote_nchini_kuomboleza_mauaji_ya_jen._soleimani
Wananchi wa Iran katika mikoa na miji mbalimbali ukiwemo mji mkuu Tehran wamemiminika mabarabarani baada ya Sala ya Ijumaa kushiriki maandamano ya kuomboleza na kulaani mauaji ya kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Jan 03, 2020 12:32 UTC
  • Wairani waandamana kote nchini kuomboleza mauaji ya Jen. Soleimani

Wananchi wa Iran katika mikoa na miji mbalimbali ukiwemo mji mkuu Tehran wamemiminika mabarabarani baada ya Sala ya Ijumaa kushiriki maandamano ya kuomboleza na kulaani mauaji ya kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran.

Makumi ya maelfu ya Wairani wameshiriki maandamano hayo katika mji mtakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran na pia katika mkoa wa Kerman, kusini mashariki mwa nchi.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye picha zinazomuonyesha Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa shahidi katika shambulizi la kigadi la Marekani nchini Iraq.

Kadhalika waandamanaji hao wa Kiirani wamesikika wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Utawala wa Kizayuni wa Israel.'

Maelfu ya Wairani katika maandamano ya leo Ijumaa

Katika hatua nyingine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita Balozi Mdogo wa Uswisi mjini Tehran; nchi ya Ulaya inayowakilishia maslahi ya Marekani hapa nchini, na kumkabidhi malalamiko rasmi ya Tehran juu ya mauai ya Jenerali Soleimani.

Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mambo ye Nje ya Iran amesema balozi huyo wa Uswisi hapa Tehran amekabidhiwa malalamiko hayo leo Ijumaa na kuarifiwa kuwa, "Hatua hiyo ya Marekani ni ugaidi wa wazi wa kiserikali na kwamba utawala wa Washington utabeba dhima ya matokeo mabaya ya kitendo hicho."