Kuuawa shahidi Meja Jenerali Qassim Solaimani; ahadi ya kweli iliyotimia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58292
Meja Jenerali, Qassim Solaimani, Meja Jenerali shahidi Qassim Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (SEPAH), aliuawa shahidi usiku wa kuamkia jana Ijumaa katika shambulio la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mji mkuu wa Iraq.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jan 04, 2020 02:39 UTC
  • Kuuawa shahidi Meja Jenerali Qassim Solaimani; ahadi ya kweli iliyotimia

Meja Jenerali, Qassim Solaimani, Meja Jenerali shahidi Qassim Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (SEPAH), aliuawa shahidi usiku wa kuamkia jana Ijumaa katika shambulio la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mji mkuu wa Iraq.

Meja Jenerali Solaimani alizaliwa tarehe 13 Machi 1957 katika viunga vya mji wa Kerman ulioko kusini mwa Iran. Katika kipindi cha vita vya vya kulazimishwa Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein, shahidi Solaimani alikuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah mjini Kerman. Baada ya kumalizika vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran, Meja Jenerali Solaimani alijihusisha na mapambano dhidi ya wafanya magendo na makundi ya uhalifu katika maeneo ya mashariki mwa Iran.

Katika kipindi hicho, shahidi Solaimani alifanikiwa kuwaangamiza wanachama wengi wa magenge ya uhalifu yaliyokuwa chanzo cha ukosefu wa usalama mashariki mwa Iran na kuweza kurejesha usalama na utulivu katika mipaka ya mashariki mwa nchi. Mwaka 1997 aliteuliwa kuchukua wadhifa wa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kuhitimisha nguvu za kundi la kigaidi la Taliban na makundi mengine yaliyokuwa chanzo cha ukosefu wa amani na usalama mashariki mwa Iran.

Shahidi Qassim Solaimani

Sambamba na kuanza jinai za kundi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq, mwanamapambano huyo aliweza kuwa na nafasi muhimu mno katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi na kurejesha amani na utulivu katika nchi hizo. Kuuawa shahidi, Meja Jenerali Qassim Solaimani, kumelaaniwa na kunaendelea kulaaniwa katika maeneo mbalimbali ya dunia. Viongozi wa dunia wakiwemo hata baadhi ya waitifaki wa Marekani wameendelea kukosoa hatua hiyo ya kichokozi ya Marekani ya kumuua mwanamapambano huyo.

Wananchi wa Iran katika mikoa na miji mbalimbali ukiwemo mji mkuu Tehran jana walimiminika mabarabarani baada ya Swala ya Ijumaa kushiriki maandamano ya kuomboleza na kulaani mauaji ya kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana alitangaza siku tatu za maombolezo hapa nchini baada ya kuuawa shahidi Qassim Solaimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Katika salamu zake rambirambi kutokana na kuuliwa shahidi Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa: Kisasi kikali kinawasubiri watenda jinai ambao mikono yao michafu imemwaga damu yake na mashahidi wengine katika shambulizi la usiku wa kuamkia jana.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa jana hapa mjini Tehran ameashiria juu ya kuuliwa shahidi Meja Jenerali Qassim Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na kusisitiza kuwa, Wamarekani katu hawataonja tena ladha ya amani popote duniani kufuatia ukatili huo.

Kwa upandewake, Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Meja Jenerali Qassim alikuwa mtu mwenye taathira kubwa mno katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi ya Daesh, al-Nusra, al-Qaeda na mengineyo na amekuwa mlengwa wa ‘ugaidi wa kimataifa wa Marekani’.

Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Sayyid Ebrahim Raisi ametoa ujumbe akilaani jinai ya Marekani ya kumuua shahidi Meja Jenerali Qassim Soleimani na kusema kuwa: Japokuwa kambi ya muqawama na mapambano imeumizwa na mauaji ya Shahidi Soleimani na mwana jihadi mwenzake, Abu Mahdi al Muhandes, lakini hapana shaka kuwa, kila tone la damu zao litatengeneza mamia ya Qassim Soleimani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa, Tehran italipiza kisasi kwa wale wote waliohusika na mauaji ya Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), Meja Jenerali Qassem Solaimani. Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema kuwa, jinai hii kubwa ambayo ni ushahidi mwingine wa uhabithi wa Marekani na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na huko Iraq, itapatiwa jibu kali.