Jan 05, 2020 15:40 UTC

Mwili wa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ya mashahidi wenzake waliouliwa shahidi pamoja naye katika jinai ya kinyama iliyofanywa na majeshi ya kigaidi ya Marekani imesindikizwa na kuagwa leo katika mji mtakatifu wa Mashhad kaskazini mwa Iran na huko Ahvaz kusini mwa nchi.

Shughuli ya maombolezo ya kuisindikiza na kuiaga miili ya mashahidi hao katika mji wa Mashhad imehudhuriwa na mamilioni ya wananchi wa mkoa wa Khorasan Razavi wakiwemo viongozi kadhaa.

Katika shughuli hiyo ya maombolezo, wananchi wa Iran walipiga nara na sha'ar mbali mbali, wakiwa wamebeba pia picha na mabango kumuenzi na kumkumbuka shahidi kamanda Qassem Soleimani na mashahidi wenzake.

Shahidi Qassem Soleimani (kushoto) akiwa na shahidi Abu Mahdi Al-Muhandis

Baada ya shughuli maalumu ya kisomo na dua iliyofanyika katika haram ya Imam Ridha (as), Imamu wa nane wa Waislamu wa Kishia, mwili wa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na ya mashahidi wenzake ilisafirishwa kuletwa mjini Tehran.

Miili ya mashahidi hao wa mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na majeshi ya kigaidi ya Marekani nchini Iraq inatazamiwa kusindikizwa na kuagwa hapa mjini Tehran na katika mjii wa Qum hapo kesho.

Maziko ya shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yatafanyika siku ya Jumanne mahali alikozaliwa mkoani Kerman, kusini mwa Iran.

Leo asubuhi, mwili wa shahidi Qassem Soleimani na ya wanamapambano wenzake ilisindikizwa na kuagwa katika mji wa Ahvaz kusini mwa Iran, mara baada ya kuwasili nchini kutoka Iraq.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na watu wanane wengine waliuawa shahidi usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa katika shambulio la kigaidi la anga lililofanywa na majeshi vamizi na ya kigaidi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.../

Tags