Mousavi: Ndoto za Trump za kufikia mapatano mapya na Iran hazitoaguka
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ndoto ya rais wa Marekani, Donald Trump ya kuikia makubaliano mapya na Iran itaendelea kubakia kuwa ndoto isiyoagulika.
Majibu hayo yametolewa baada ya Brian Hook mkuu wa kundi la kuchukua hatua dhidi ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuliambia gazeti la al Sharq al Awsat jana Alkhanisi mjini Davos Uswisi kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametoa pendekezo la kufikiwa makubaliano mapya yasiyo ya JCPOA akisema kuwa makubaliano hayo mapya itabidi yaizuie Iran kurutubisha urani, iache kufanyia majaribio makombora yake na isiyaunge mkono makundi na nchi zinazoipinga Marekani na Israel katika eneo hili.
Kabla ya hapo Boris Johnson alikuwa amesema kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA inabidi yabadilishwe na nafasi yake ichukuliwe na mapatano ya Trump.

Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje imejibu kwa kusema kuwa, hizo zitabakia kuwa ndoto zisizoagulika.
Sayyid Abbas Mousavi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter jana Alkhamisi kwamba, hatua ya Brian Hook ya kuonesha hadharani mpango alioupa jina la "Makubaliano ya Trump" ni ndoto tu ambayo inatokana na kiburi na kujiona bora viongozi hao wa Marekani kuliko watu wengine duniani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ametoa msemo maarufu wa Kiirani unaosema: "Amekosa ngano ya Rey na tende za Baghdad" akikusudia kwamba "mtaka yote hukosa yote."