Feb 25, 2020 07:56 UTC
  • Nchi zilizoliwekea taifa la Iran vikwazo vya madawa ni katili

Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi ambazo zinazuia madawa kuingia hapa nchini ni katili na wauaji wa binadamu.

Ali Baqeri-Kani alisema hayo jana Jumatatu katika Mkutano wa 43 wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi na kuongeza kuwa, nchi zilizoiwekea Iran vikwazo vya dawa hazipaswi kuwa wanachama wa baraza hilo.

Ameashiria kuhusu vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran na kubainisha kuwa, "taifa la Iran ni moja wa wahanga wa vikwazo vya Marekani vinavyokiuka haki za binadamu kwa mpangilio maalumu."

Ali Baqeri-Kani ameeleza bayana kuwa, sera mpya ya mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani dhidi ya Iran imesababisha watu wenye mahitaji washindwe kufikiwa na dawa na vitu vingine vya msingi, huku akipinga madai ya Washington kuwa madawa si sehemu ya bidhaa ilizoziwekea vikwazo.

Watoto wa Kiirani ni miongoni wa wagonjwa wa saratani wanaokosa dawa na matibabu kutokana na vikwazo

Kadhalika Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezikosoa vikali nchi zinazofuata kibubusa sera hiyo ya Marekani ya kulibana taifa la Iran kwa vikwazo akisisitiza kuwa, zinafanya hivyo kwa kutanguliza maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa bila kuzingatia masuala ya haki za binadamu.

Amesema, "vitendo hivi si tu vinaliadhibu taifa zima, lakini pia mtindo mpya wa kukanyaga haki za binadamu, jambo ambalo linapaswa kuwekwa kama ajenda kuu ya mkutano wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la UN." 

 

Tags