Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Iran yaadhimishwa nchini
Leo Jumatano tarehe 8 Aprili sawa na tarehe 20 Farvardin imepewa jina la "Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia" katika kutambua jitihada za kujivunia za wasomi wa nyuklia wa Iran katika kukamilisha mzunguko wa utengenezaji wa fueli ya nyuklia.
Wasomi na Wanasayansi wa Kiirani katika siku kama hii ya leo mnamo mwaka 2006 walifanikiwa kutengeneza mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia katika maabara. Baada ya kutangazwa habari ya mafanikio hayo ya wasomi na wanasayansi Wairani katika urutubishaji urani na kuzinduliwa mchakato kamili wa urutubishaji urani kwa kutumia mashinepewa au centrifuge zilizoundwa nchini Iran, Shirika la Kimataifa la Nishati Atomiki IAEA liliitangaza Iran kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimeweza kumiliki teknolojia ya kurutubisha urani katika uga wa shughuli za nyuklia kwa malengo ya amani.
Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran jana Jumanne alituma ujumbe kwa mnasaba wa kukaribia Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia na kuashiria kuzinduliwa mafanikio mapya 122 ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yenye kutia matumaini ni mwanzo wa ukurasa mpya katika ustawi wa pande zote wa miradi ya kujivunia ya Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran.
Salehi amebainisha kuwa katika hali ya vikwazo vya kidhulma vya uistikbari wa dunia dhidi ya Iran ya Kiislamu; Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran inalihesabu suala la kudhamini mahitaji ya kitiba kuwa jukumu la kitaifa na kiakhlaqi na kuongeza kuwa: Kuzidishwa pakubwa uzalishaji na huduma zinazohusiana na sekta ya matibabu ya kinyuklia na kuvidhaminia mahitaji ya dawa vituo vya tiba na afya hapa nchini Iran kunafanyika kwa kiwango cha juu na kwa kasi inayokubalika.