"Marekani inazitishia IAEA na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa"
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran vinapaswa kutamatishwa muda wake utakapofika kama sehemu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya vitisho vya Marekani kwa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki (IAEA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumapili katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa jijini Tehran na kusisitiza kuwa, taifa hili litatoa jibu muafaka iwapo Marekani itapika njama za kuzuia kuondolewa kwa marafuku hiyo ya silaha dhidi ya Iran muda wake utakapomalizika Oktoba mwaka huu.
Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, "kufutwa marufuku ya silaha dhidi ya Iran ni moja ya mafanikio muhimu ya JCPOA, na iwapo Marekani inataka kuvuruga mafanikio haya, nchi nyingine zinafahamu jibu tutakalolitoa."
Amekosoa kitendo cha Marekani cha kuzitishia Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki (IAEA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa maslahi ya Washington na kubainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu mwafaka iwapo kipengee hicho muhimu cha kuondolewa Iran vikwazo vya silaha kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN kitakiukwa.
Kadhalika Rais wa Iran amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuushinikiza Mfuko wa Fedha Duniani (IMF) ili usiipe Jamhuri ya Kiislamu mkopo wa dola bilioni 5 inazohitaji kwa ajili ya kupambana na janga la corona.
Itakumbukwa kuwa Iran iliwasilisha ombi lake la mkopo wa dola bilioni 5 kwa IMF ili kuiwezesha kukabiliana na maambukizo ya corona, lakini Marekani imekuwa ikifanya jitihada za kukwamisha mkopo huo.