Jun 28, 2020 07:36 UTC
  • Zarif: Marekani haiheshimu haki yoyote ya binadamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani imeshindwa kuheshimu haki zozote za msingi za binadamu, na imefanya hivyo kuanzia kuupa utawala wa Iraq silaha za kemikali dhidi ya Iran hadi kuliwekea vikwazo na kulifanyia ugaidi wa kiuchumi taifa la Iran.

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana Jumamosi katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya shambulizi la silaha za kemikali lililofanywa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein dhidi ya mji wa Sardasht katika mkoa wa Azerbaijan, huko magharibi mwa Iran.

Dakta Zarif ameashiria kuhusu rekodi nyeusi ya jinai za Marekani dhidi ya Iran na mataifa mengine ya eneo la Asia Magharibi na kusema, "taifa la Iran limeshuhudia wazi hatua hizo za jinai za Marekani kuanzia katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, vita vya kiuchumi, ugaidi wa kiuchumi na ugadi wa kiserikali."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza bayana kuwa, taifa la Iran kamwe halitasahau shambulizi la silaha za kemikali dhidi ya mji wa Sardash mwaka 1987, hujuma ya kikatili iliyofanywa na Saddam kwa kutumia zana na silaha angamizi alizopewa na Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia na Uholanzi.

Baadhi ya wahanga wa shambulizi la silaha za kemikali ya sumu mjini Sardasht miaka 33 iliyopita

Itakumbukwa kuwa, miaka 33 iliyopita katika siku kama ya jana, mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein. 

Mbali na hayo, Wairani wengine 2,600 wakiwemo askari waliuawa kwa silaha hizo za kemikali katika vita vya Iraq dhidi ya Iran kuanzia mwaka 1980 hadi 1988, mbali na wengine 107,000 kujeruhiwa au kupata ulemavu wa daima.

Tags