Sep 15, 2020 08:12 UTC
  • Zarif: Trump anawatumia watawala vibaraka wa Kiarabu kama chombo cha kampeni

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jitihada zinazofanywa na Rais Donald Trump wa Marekani za kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya utawala haramu wa Israel na nchi kadhaa za Kiarabu zinaashiria wazi kuwa mwanasiasa huyo wa chama cha Republican anataka kutumia hatua hiyo kama wenzo wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka huu.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Donald Trump ana hamu kubwa ya kupata picha ya kampeni. Mkwewe (Jared Kushner) amewarubuni wateja wao katika eneo wampe (picha) moja.

Dakta Zarif ameukejeli utiaji saini wa makubaliano hayo na kuyataja kama 'mapinduzi ya kidiplomasia' na kwamba huu ndio mwanzo tu wa watawala vibaraka wa Kiarabu kudhihirisha uhalisia wao.

Amesema hakuna jipya katika utiaji saini huo kwa kuwa tawala hizo za Kiarabu zimekuwa na uhusiano wa siri na utawala haramu wa Israel, na kinachofanyika hivi sasa ni kuudhirisha tu kwa walimwengu.

Usaliti wa Imarati na Bahrain umekabiliwa na upinzani mkali ndani na nje ya eneo la Asia Magharibi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza bayana kuwa, "makubaliano yanayosainiwa si kati ya maadui, bali ni baina ya waitifaki wa muda mrefu."

Hapo jana pia, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu alisema hatua hiyo Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni upuuzaji na khiyana kwa malengo ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Tags