Iran yaadhimisha Siku ya Kufungamana na Watoto wa Palestina
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumatano ya Septemba 30 (tarehe 9 Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia), imeadhimisha Siku ya Kufungamana na Watoto wa Kipalestina.
Siku hii ilipewa jina la siku ya kufungamana na kuonyesha mshikamano kwa watoto na vijana wa Kipalestina, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mauaji ya kinyama dhidi ya Muhammad al-Durrah kijana mdogo wa Kipalestina aliyeuawa shahidi na askari katili wa Israel mnamo Septemba 30 mwaka 2000.
Mauaji hayo ya kijana wa miaka 12 yalikuwa kama mlipuko wa bomu katika vyombo vya habari ulimwenguni na fikra za waliowengi duniani, na yanaendelea kulaani hadi leo hii.
Siku mbili baada ya kuanza Intifadha ya al-Aqsa Septemba mwaka 2000, Muhammad al-Durrah akiwa pamoja na baba yake walikuwa katika eneo la Netzarim katika Ukanda wa Gaza na walikuwa na nia ya kuelekea nyumbani kwao, aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi wakati alipokuwa amejificha nyuma ya baba yake ili asipatwe na risasi.
Tukio hilo lilirekodiwa na mpiga picha wa Kanali ya 2 ya Kiarabu ya Ufaransa na kisha likarushwa hewani na runinga hiyo. Baadaye mkanda wa tukio hilo la kinyama ukaonyeshwa kwa wingi katika vyombo mbalimbali vya habari ulimwenguni.
Kuuawa kinyama Muhammad al-Durrah kijana mdogo wa Kipalestina, ni sehemu ndogo mno ya maelfu ya jinai za Israel ambazo zimefanya na Wazayuni makatili katika kipindi cha zaidi ya miongo sita ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina ambayo ilishuhudiwa na walimwengu.