Rouhani: Mdahalo wa Urais umefichua matatizo yanayoikabili Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mdahalo wa kwanza wa wagombea wawili wa urais katika uchaguzi utakaofanyika Novemba mwaka huu nchini Marekani, Donald Trump wa chama cha Rebulican na Joe Biden wa Democratic umefichua kina cha matatizo na changamoto zinazoikabili serikali ya Washington.
Rais Rouhani amesema mdahalo huo uliogubikwa na cheche za maneno makali, tuhuma na matusi umeanika namna Marekani ilivyofeli katika sera zake za ndani na za kigeni.
Dakta Rouhani amesema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa jijini Tehran na kubainisha kuwa, "mbali na Washington kufeli kupata ushindi wowote katika uga wa kimataifa, lakini pia imeshindwa vibaya katika uga wa kupambana na janga la corona, ukosefu mkubwa wa ajira, na kushtadi machafuko ndani ya Marekani."
Amesema "Wamarekani wameshindwa kufikia malengo yao mkabala wa Iran, eneo la Asia Magharibi, eneo la Pacific, Ulaya na Mkataba wa Biashara Huru Amerika ya Kaskazini (NAFTA). Kwa ujumla sera zao za kigeni zimegonga mwamba."
Rais Rouhani amesema ni jambo la kawaida kwa Marekani kujaribu kuficha matatizo ya ndani kwa walimwengu, na ndio maana inapanga njama kila kukicha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameeleza bayana kuwa, "hii leo, Marekani inatumia sera zilizojaa uhasama zaidi, za jinai na zinazofanana na za kigaidi dhidi ya taifa la Iran lenye jamii ya watu zaidi ya milioni 84."
Hata hivyo Rais wa Iran amesisitiza kuwa, njama hizo zilizojaa uadui za Marekani dhidi ya Iran zitaendelea kugonga mwamba tu.