Iran yaionya Marekani dhidi ya mahesabu ghalati
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ya Iran amesema kuwa mahesabu yasiyo sahihi ya Marekani ndiyo sababu ya kushindwa kwake mbele ya taifa la Iran tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo Ijumaa katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kueleza bayana kuwa, "Marekani kwa mara kadhaa imejaribu kuchukua hatua zilizo dhidi ya taifa na serikali ya Iran tangu baada ya Mapinduzi ya (Kiislamu) mwaka 1979, lakini mara zote imekuwa ikifeli."
Amesema mahesabu yoyote ghalati yatakuwa na matokea mabaya kwa maadui wa taifa la Iran. Khatibzadeh amebainisha kuwa: Tumewaonya Wamarekani kwamba, hatua zozote zisizo sahihi mkabala wa Iran zitawatumbukiza katika 'mama wa vinamasi.'
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ya Iran ameashiria jitihada zilizofeli za dola hilo la kiistikbari katika uwepo wake haramu katika eneo la Asia Magharibi na kusema, "makosa makubwa yaliyofanywa na Marekani ndiyo sababu ya kuufanya utawala wa Washington ushindwe, ufeli na utimuliwe katika eneo."
Kuhusu njama iliyofeli ya Marekani ya kutaka kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, Khatibzadeh amebainisha kuwa, kile ambacho Washington imekuwa ikifanya katika utawala wa Donald Trump ni kuileta pamoja na kuiunganisha jamii ya kimataifa dhidi ya Marekani.
Ameashiria kauli ya vitisho inayotolewa mara kwa mara na watawala wa Marekani kwamba machaguo yote yako mezani na kueleza bayana kuwa, "kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujihami dhidi ya ukiukaji wowote wa mamlaka yake ya kujitawala, mipaka na maslahi ya taifa."