Nov 08, 2020 02:37 UTC
  • Spika Qalibaf asisitiza nchi za eneo kushirikiana ili kuutokomeza ugaidi

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililolenga wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kabul nchini Afghanistan na kusisitizia ulazima wa nchi za eneo kushirikiana pamoja ili kuutokomeza ugaidi.

Katika ujumbe kwa Mir Rahman Rahmani, Spika wa Bunge la Afghanistan, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Baqir Qalibaf ametoa mkono wa pole kwa wananchi, serikali na waathirika wa tukio hilo la kigaidi na kusisitiza kwamba, vitendo hivyo havitateteresha irada ya taifa imara la Afghanistan kuelekea kwenye amani, ustawi na kuimarisha usalama na uthabiti.

Katika ujumbe wake huo, Qalibaf amesisitiza kuwa, umoja, mtazamo wa pamoja na ushirikiano wa nchi za eneo unaweza kung'oa mizizi ya ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka na akaongeza kwamba, mtazamo huo wa pamoja na ushirikiano unaweza kuzuia kutokea tena jinai kama hizo zinazovuruga amani na usalama.

Athari za shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Kabul

Siku ya Jumatatu iliyopita, watu watatu wenye silaha walivamia Chuo Kikuu cha Kabul, ambapo baada ya kuripua bomu walianza kuwafyatulia risasi wanachuo wa chuo hicho. Wanachuo 22 waliuawa na wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa katika shambulio hilo la kinyama.../

Tags