Ayatullah Raisi: Fedheha na kuumbuka Marekani kumedhihirika wazi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64663-ayatullah_raisi_fedheha_na_kuumbuka_marekani_kumedhihirika_wazi
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran ameashiria matukio ya hivi karibuni nchini Marekani baada ya kufanyika uchaguzi na kusema kuwa, fedheha ya Marekani imedhihirika wazi.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Nov 16, 2020 07:38 UTC
  • Ayatullah Raisi: Fedheha na kuumbuka Marekani kumedhihirika wazi

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran ameashiria matukio ya hivi karibuni nchini Marekani baada ya kufanyika uchaguzi na kusema kuwa, fedheha ya Marekani imedhihirika wazi.

Ayatullah Ebrahim Raisi amesema kuwa, kile kinachoshuhudiwa leo nchini Marekani ni fedheha na kuumbuka vibaya kabisa Marekani ambayo baada ya kuonyesha sura bandia kwa muda mrefu kuhusu demokrasia sasa sura yake halisi imedhihirika mbele ya macho ya walimwengu.

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, katika uchaguzi wa Rais uliofanyika hivi karibuni nchini Marekani, walimwengu wote wameshuhudia kwa macho yao kwamba, kile ambacho hadi sasa Marekani ilikuwa ikijaribu kukipigia debe na kuwaonyesha walimwengu kuhusiana na sura yake kilikuwa ni kiiini macho tu na sura isiyo halisi kabisa ya nchi hiyo.

Joe Biden na Donald Trump wagombea wawili wa kiti cha Urais nchini Marekani

 

Kadhalika Ayatullah Raisi amebainisha kwamba, Marekani siku zote imekuwa ikifanya hima ya kutoa vitisho na kupotosha mambo ili ipate nafasi ya kudhibiti na kuzitawala fikra na mitazamo ya jamii mbalimbali ulimwenguni.

Mkuu huyo wa Idara ya Mahakama nchini Iran ameashiria kusimama kidete wananchi wa Iran mbele ya maadui na kubainisha kwamba, ujumbe wa wananchi wa taifa hili, ni kusimama kidete, kudumisha muqawama, kutotetereka na kuzalisha bidhaa muhimu katika uga wa usalama na uchumi ambazo zitazidi kulifanya taifa hili la Kiislamu kuwa imara, madhubuti na lenye nguvu siku baada ya siku.