Wimbi la maambukizo ya corona limeanza kupungua nchini Iran
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona nchini Iran amesema kuwa, takwimu za karibuni kabisa zinaonesha kuwa wagonjwa wa COVID-19 wanaoripoti katika vituo vya matibabu humu nchini wamepungua kwa asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na wiki iliyopita.
Masoud Mardani amesema hayo mapema leo Jumanne katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran wameonesha ushirikiano mzuri katika kuchunga protokali za afya na kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya kirusi cha corona humu nchini.
Amesema, Alhamdulillah mpango wa kukabiliana na COVID-19 umeonesha matunda mazuri hadi hivi sasa lakini matokeo yake halisi yataonekana baada ya takriban wiki tatu za utekelezaji wa mpango huu mpya wa kukabiliana na ugonjwa huo humu nchini.
Sheria mpya za kukabiliana na COVID-19 zilianza kutekelezwa Jumamosi wiki hii na zinatarajiwa kuendelea kwa muda wa wiki mbili.
Huku hayo yakiripotiwa, Mkuu wa Kamati ya Kielimu ya Kupambana na Corona nchini Iran amesema kuwa, mashirika kadhaa humu nchini hivi sasa yanafanya juhudi za kutengeneza kizazi kipya cha chanjo za corona zinazotumia utaalamu wa MRNA.
Mustafa Ghanei alisema hayo jana na kutoa ufafanuzi kuhusu zinavyofanya kazi chanjo za MRNA au RNA akisema kuwa, jeni za RNA zinapoingizwa kwenye mwili wa mwanadamu zinazijulisha seli za mwili huo protini zipi ni virusi na kuuchochea mwili kutengeneza seli na "antibodi" za kujikinga na maradhi.